0

Mvua kubwa zasababisha mafuriko Kenya na Tanzania

Mvua kubwa zasababisha mafuriko Kenya na Tanzania 
 
Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika ukanda wa Afrika Mashariki imesababisha vifo, hasara na mali na mafuriko katika nchi za Kenya na Tanzania.

Wakazi wa miji ya Dar es Salaam nchini Tanzania na Nairobi Kenya wanakumbwa na adha kubwa hasa ya usafiri kutokana na barabara kujaa maji na kuharibika baadhi ya miundo mbinu. Mvua kubwa iliyonesha jana katika jiji la Dar es Salaam ilisababisha adha kubwa kwa wakazi wa mji huo kutokana na barabara nyingi kujaa maji na kusababisha usumbufu mkubwa kutokana na msongamano mkubwa wa magari.

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wamebakia bila makazi hasa katika maeneo ya Bunju nje kidogo ya mji kutokana na nyumba zao kubomolewa na mafuriko.

katika baadhi ya mikoa pia kunaripotiwa hali kama hiyo huku mkoa wa Morogoro ukionekana kuathirika zaidi. Tayari watu kadhaa wameripotiwa kufariki duniani mkoani humo kutokana na maafa ya mafuriko.

Nchini Kenya pia hasa katika jiji la Nairobi hali haiko tofauti na Dar es Salaam kwani baadhi ya barabara hata ile ya kisasa ya Thika Super Highway nayo ilijaa maji na kusababisha usumbufu mkubwa. Utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa, katika siku za usoni jiji la Nairobi na maeneo mengine ya Kenya yatashuhudia mvua kubwa.

Post a Comment

 
Top