zilizotokana na makubaliano ya waasisi wa taifa ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Abeid Amaan Karume ambao lengo lao lilikuwa ni kuwa na taifa moja lenye nguvu kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Historia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaanzia Aprili 26 mwaka 1964 siku ambayo nchi ya Jamhuri ya Tanganyika ambayo kwa sasa ni Tanzania bara pamoja na iliyokuwa Jamhuri ya Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja) ziliungana na kuwa nchi moja ikiwa ni siku 100 tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na Nyerere na Karume, Aprili 22, mwaka 1964, visiwani Zanzibar.
Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili 26 na Aprili 27, mwaka 1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati za Muungano. Sheria za Muungano zilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zililazimika, kuwa dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jina ambalo lilibadilishwa Oktoba 28, mwaka 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tangu makubaliano hayo, taifa la Tanzania linalojumuisha Watanganyika na Wanzazibar lilianza kujiendesha kwa umoja na mshikamano huku msingi wake mkuu ukiwa ni kudumisha umoja, amani na mshikamano baina ya Watanzania na taifa hilo kwa ujumla. Kimsingi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unabaki kuwa ni fahari ya Watanzania, kwani mwelekeo wa dunia katika nyanja mbalimbali, mataifa kuungana kwa ushirikiano wa aina mbalimbali ni muhimu kuliko taifa moja kupambana kivyake.
Hata hivyo, kama ulivyo ushirikiano wowote, haukosi kukumbwa na matatizo, hivyo ndivyo ilivyo kwa muungano huu wa Tanzania ambao hadi kufikia miaka hiyo 52, umekuwa ukikumbwa na matatizo kadhaa na kuufanya kuwa muungano wenye mapito mengi. Si muungano huo pekee wa Tanzania ndio ulio na matatizo kwani vivyo hivyo muungano mwingine kama vile ya United Kingdom (UK), Uingereza na United States of America (USA) kwa maana ya Marekani na United Arabs Emirate (UAE), nayo ina matatizo, lakini hadi leo inaendelea kudumu.
Kwa Tanzania moja ya mapito yanayoukabili muungano huo ni kero za muda mrefu za muungano ambazo Serikali ya Tanzania imekuwa katika jitihada za kuhakikisha kero hizo zinapatiwa ufumbuzi. Kero hizo za muungano ziliibuka baada ya kuzaliwa kwa muungano huo kutokana na malalamiko ya watu wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliyaweka mambo 11 chini ya Serikali ya Tanzania. Mambo hayo ni pamoja na Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya nchi za Nje, ulinzi, Polisi, mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya usalama, uraia, uhamiaji na mikopo na biashara za nje. Mengine ni utumishi katika Serikali ya muungano, kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha, bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.
Hata hivyo, ukweli mambo hayo 11 baadaye yalikuja kuongezwa na kufikia 22 hali iliyosababisha kuzaliwa kwa kero zaidi za Muungano. Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba, anasema katika kuhakikisha changamoto za Muungano zinatatuliwa, Serikali ilianzisha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Maagizo hayo yalitolewa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, mwaka 2006 na kuwataka Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi kutoka Serikali ya Zanzibar kukutana na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazoukabili Muungano. Anasema katika kipindi hicho Ofisi ya Makamu wa Rais iliratibu vikao viwili kati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa SMZ Mei 22, mwaka 2006, Dar es Salaam na Novemba 21, mwaka 2006, Zanzibar.
“Hata hivyo, Februari mwaka 2008, Rais Kikwete alifanya marekebisho ya kiutendaji serikalini ambapo Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zanzibar katika kushughulikia masuala ya Muungano iliwekwa chini ya Uongozi na Uenyekiti wa Makamu wa Rais,” anasema. Anasema kwa kuzingatia utaratibu huo, kikao cha kwanza chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais kilifanyika Mei 15 mwaka 2008, Dar es Salaam, na vilivyofuata vilikuwa ni: Oktoba 11, mwaka 2008, Zanzibar; Mei 19, mwaka 2009, Dar es Salaam; Juni2, mwaka 2010, Zanzibar; Januari 28, mwaka 2012, Dar es Salaam; Januari 13 , mwaka 2013, Zanzibar na Juni 23 , mwaka 2013, Dodoma.
January anasema kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 jumla ya hoja 15 ziliwasilishwa na kujadiliwa na Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ. Kati ya hizo, hoja 12 zimepatiwa ufumbuzi na hoja tatu zipo katika hatua mbalimbali ya kutafutiwa ufumbuzi ambazo ni masuala ya kodi, mahusiano ya kifedha na usajili wa vyombo vya moto. Anabainisha baadhi ya kero zilizopatiwa ufumbuzi kuwa ni Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura Namba 391 inayosimamiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilikuwa haitekelezwi Zanzibar kwa kuwa haikuwa suala la Muungano.
Aidha sheria hiyo pia haimshirikishi Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye dhamana ya mambo ya Haki za Binadamu. Anasema tayari hatua za kukabili changamoto hiyo zimechukuliwa na baada ya majadiliano katika vikao vya kamati ya pamoja, suala hilo limepatiwa ufumbuzi kwani Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba nane ya mwaka 2006.
Sasa sheria hiyo ni ya Muungano na Tume inafanya kazi pande zote mbili za Muungano. Anasema kutokana na maridhiano hayo, Hati ya makubaliano ilisainiwa na mawaziri husika kutoka serikali zote mbili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zanzibar kilichofanyika Juni 2, mwaka 2010, Zanzibar. Kero nyingine ni kitendo cha Zanzibar kushindwa kujiunga na Shirika la Usafiri wa Baharini (IMO) kwa kuwa kutokana na visiwa hivyo kuwa sehemu ya Tanzania havikuwa na sifa ya kuwa dola na kuweza kuwa mwanachama wa shirika hilo.
Anasema kutokana na hali hiyo, Zanzibar ilikuwa na sheria yake ya usafiri baharini ya mwaka 2006 ambayo imekuwa ikitumika kwa masuala yote yanayohusu uchukuzi na usalama wa njia ya majini katika mikataba yote ya SMZ. Aidha, ilikuwa na mpango wa kuanzisha chombo chake cha kusimamia masuala ya usafiri majini hli iliyozusha utata wakati Zanzibar ilipoomba uanachama kwenye taasisi hiyo ya IMO.
Anafafanua kuwa ingawa uanachama wa ‘IMO’ ni wa kitaifa, baada ya mashauriano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ‘IMO’, imekubalika Zanzibar kuwa na mamlaka yake ya usafiri majini ambayo itatekeleza baadhi ya majukumu kulingana na mikataba ya kimataifa. “Hoja hii imepatiwa ufumbuzi na Hati ya makubaliano imesainiwa na mawaziri husika kutoka serikali zote mbili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika Juni 2, mwaka 2010, Zanzibar.
Kuhusu kero ya uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari, Waziri January anasema ukanda wa uchumi wa bahari kuu unasimamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia sheria ya Mamlaka ya Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari kuu. Anasema : Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu ilikuwa haitekelezwi Zanzibar kutokana na kutozihusisha taasisi za SMZ zinazoshughulikia masuala ya Uvuvi katika Bahari Kuu katika utekelezaji wake.
Hata hivyo, anabainisha kuwa baada ya majadiliano, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho Februari, mwaka 2007 kupitia Sheria Nya mwaka 2007 na kuzitambua taasisi zinazohusika na matumizi ya Bahari Kuu kwa upande wa Zanzibar na kuzijumuisha katika Kamati ya Utendaji ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu hivyo, kuiwezesha mamlaka kuanza kazi zake rasmi mwaka 2010.
Anasema kwa sasa Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ni moja, na Makao Makuu yake yako katika kijiji cha Fumba Zanzibar. Mamlaka hiyo ina majukumu ya kutoa leseni za uvuvi katika bahari kuu, kudhibiti viwango vya uvuvi, kusimamia rasilimali ya uvuvi na hifadhi ya mazingira ya bahari na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi katika bahari kuu, anafafanua.
Hata hivyo, Sheria hiyo bado haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi, hivyo sekta husika zimekubaliana utaratibu wa muda ili shughuli za mamlaka ziendeshwe katika utaratibu huo wa mpito hadi hapo Sheria hiyo itakaporidhiwa na Baraza la Wawakilishi. Aidha, anafafanua kuwa katika kutatua kero nyingine ya ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tayari inashiriki kikamilifu na kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo na imeshawasilisha miradi minane ya maendeleo kwa ajili ya kujumuishwa katika Miradi ya Kikanda inayotekelezwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika eneo la mgawanyo wa mapato, Waziri huyo anakiri kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikipata misaada mbalimbali kutoka kwa washirika wa maendeleo na nchi wahisani kwa ajili ya kutekeleza programu za maendeleo. Anasema kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na madai kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa haipati mgawo stahiki wa mikopo ya kibajeti inayotolewa na wahisani katika General Budget Support (GBS).
Anasema katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya SMT na SMZ imeridhiwa kwamba fomula ya asilimia 4.5 itumike katika kuhakikisha SMZ inapata fungu lake. Hivyo, kuanzia mwaka wa fedha 2009/2010 Zanzibar inanufaika na gawiwo hilo la asilimia 4.5 ya Misaada ya Kibajeti. Anataja eneo lingine la kero hizo za Muungano kuwa ni misamaha ya mikopo ya fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Anasema kulikuwa na makubaliano ya awali na IMF kuhusu matumizi ya fedha za MDRI (Multilateral Debt Relief Initiative) zitokanazo na misamaha ya mikopo ya IMF kwamba, Zanzibar itatumia fedha hizo kununua vifaa vya kutengenezea barabara, kilimo, na masuala mengine ya maendeleo. Anasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilihitaji kununua pia magari kwa ajili ya matumizi yake kupitia fedha za MDRI suala ambalo halikuwepo katika makubaliano ya awali baina ya Tanzania na IMF.
Katika kulishughulikia suala hilo Wizara ya Fedha ya SMT ilifanya mawasiliano na IMF kuangalia uwezekano wa Zanzibar kujumuisha ununuzi wa magari kati ya vitu vinavyoweza kupatikana kutoka katika msamaha huo. “Maombi hayo yalikubaliwa na suala hili limeshapatiwa ufumbuzi kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishapata fedha za misamaha hiyo na tayari ilishanunua vifaa vya kujengea barabara, vifaa vya hospitali, vifaa vya kilimo na magari kwa ajili ya matumizi ya Serikali,” anasisitiza.
Hata hivyo, katika hoja hiyo ya Mgawanyo wa Mapato, vipengele viwili vinaendelea kutafutiwa ufumbuzi ambavyo ni Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Faida ya Benki Kuu. (Angalia katika kipengele cha hoja zilizo katika hatua mbalimbali za utatuzi).
Kuhusu kodi nyingine ikiwemo lipa kadri inavyotumia, Waziri huyo anasema, kulikuwa na tatizo la Serikali ya Zanzibar kutonufaika ipasavyo na kodi ya mapato yatokanayo na mishahara ya wafanyakazi wa taasisi za Muungano waliopo Zanzibar (PAYE) pamoja na kodi ya kampuni na mashirika yanayofanya kazi Zanzibar (Withholding Tax).
Kutokana na hali hiyo, anasema kwa sasa pande zote mbili za Muungano zimekubaliana kuwa, Sheria ya Kodi irekebishwe ili mapato yanayokusanywa kutokana na mishahara ya wafanyakazi, kampuni au mashirika kwa upande wa SMZ yabaki Zanzibar na yale yanayokusanywa na SMT upande wa Tanzania Bara yabaki Tanzania Bara.
Aidha, pande zote mbili za Muungano zimekubaliana SMZ ipate asilimia 4.5 ya sehemu ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye kodi ya mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kama utaratibu wa muda na fedha hizo kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina wa SMZ wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea.
Kuhusu kero ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, anakiri kuwepo na tofauti ya ukadiriaji wa viwango vya thamani za bidhaa, na kodi ya forodha baina ya ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizoko Tanzania Bara na zile zilizoko Zanzibar kutokana na mifumo tofauti ya ukadiriaji. Anasema tofauti hiyo ilisababisha kufanywa kwa makadirio mapya ya kodi, ambayo ni ya viwango vya juu, kwa bidhaa zitokazo Zanzibar zinazoingia soko la Tanzania Bara.
“Hali hii ilileta malalamiko kwa wafanyabiashara wa Zanzibar, ambao nao wanatumia kipengele cha sheria ya kodi kinachosema kwamba; “Bidhaa zinazoingizwa nchini na kukamilisha taratibu zote za kiforodha kupitia kituo chochote rasmi cha forodha zihesabike kuwa zimeingizwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, na kwamba hakuna haja ya kufanya upya makadirio kwa bidhaa zinazoletwa Tanzania Bara,” anasema.
Anasema katika kulishughulikia suala hilo, TRA ilitengeneza mfumo mpya wa ukadiriaji ambao unathaminisha sawa bidhaa kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Mfumo huo umeanza kutumika Februari 25, mwaka 2011 katika vituo vyote vya forodha nchini na ulipaswa kutumika katika vituo vyote vya forodha vilivyopo Zanzibar.
Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anasema mfuko huo, haukumhusisha mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Kamati ya Usimamizi wa Mfuko ili kuweza kujua matumizi ya fedha na mipango ya maendeleo ya jimbo.
Anasema katika kurekebisha utata uliojitokeza kwa majimbo ya Zanzibar, SMZ imeamua kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa lengo sawa na lile la Mfuko wa Maendeleo ya jimbo kwa Wabunge wa SMT. January anasema kero hizo na nyingine nyingi kupitia kamai hizo, zimebainishwa, kuchambuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa lengo la kuhakikisha kila upande unanufaika.
Aidha anasisitiza kuwa hata suala la nafasi za ajira kwa Wazanzibari katika taasisi za Muungano ni mojawapo ya masuala ambayo yamejadiliwa katika vikao vya mashauriano. Serikali inaendelea na utaratibu wa kushughulikia kero zilizobaki ikiwemo zile zinazogusa maeneo nyeti yaliyoibuka na yanayoendelea kuibuka na kuleta utata katika eneo la muungano, ili kuweka usawa na kudumisha muungano huo udumu vizazi na vizazi.
Post a Comment