0


Mfanyabiashara wa mazao, Eliusta Peter(40),   amefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni akiwa katika  nyumba ya kulala wageni wilayani Kilombero.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea   Aprili 22  baada ya  wahudumu wa nyumba  ya wageni ya  Sayari kubaini   maiti katika chumba namba mbili.

Inadawa Aprili 20 mwanamke huyo  akiwa na kijana mmoja ambaye  jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi, walifika kwenye nyumba hiyo na kuchukua chumba kimoja wakisema  wao ni wafanyabiashara wa mazao.
 
“Mwili wa marehemu uligundulika ukiwa kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Sayari chumba namba mbili   saa 11 jioni na ulipochunguzwa ikagundulika kuwa kifo kilisababishwa maumivu ya jereha,”alisema Matei.

Mwanamke huyo  alikuwa na jeraha   kushoto mwa bega lake lililotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali

Matei  alisema kwa taarifa walizozipata  bila shaka kijana aliyekuwa naye  anahusika na mauaji hayo.

Wakati huo huo, jeshi la polisi wilayani Kilosa limemkamata Rogasian Jeremia kwa tuhuma za kumshambulia mkewe,   Faustina Sizayi(25) kwa kumkatataka kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa anajihusisha na kazi ya ulinzi wa maduka baada ya polisi kumsaka kwa muda mrefu na ndipo Aprili  24  alikamatwa  baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Post a Comment

 
Top