Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.
Kwa
mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka
2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala
gulagula”.
Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo
kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu
aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John
Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua
kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa
kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”
Hata hivyo,
wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake,
lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi
huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya
kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na
hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.
Dk
Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye
ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge,
kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa
Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya
televisheni nchini.
“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini.
Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo
asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.
Mjadala
huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa
taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na
Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli
hiyo ya naibu spika.
“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa
kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na
wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,” alisema Nape
kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
kuingilia kati.
Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba?
Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?
Msigwa:
Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita
mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na
akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.
Mkazi
huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani
wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni
bwege.
Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi
kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha
makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni
serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa
muhimu.
Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa
viti maalumu (Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na
kumponda Nape na uamuzi wa Serikali.
Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa.
“Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape vuvuzela,” alisema.
“Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa moja?”
Wakizungumzia
tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema
Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno
mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na
taratibu za kibunge.
“Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji.
Alisema
mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge
hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria.
Mbunge
wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na
Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi,
taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo
lolote, hii si sawa kabisa.”
Alisema Bunge linapaswa kuongozwa
kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo inawafanya wabunge wa CCM
waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani.
“Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema.
Kwa
takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa vyama
vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi
ya Rais na kurejesha uhai kwenye chombo hicho.
Katika hoja zao
jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu ya Tano
kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa kusitisha
matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa mara
kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni za
Bunge.
Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa
ufafanuzi wao, walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa
Konde (CUF), Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa
maelezo kuwa ndiye aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo.
Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala
bora na unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala
bora.
“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana
nzima ya utawala bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa
ufanisi, tija na kwa uwazi, uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa
watu kwa kufuata utawala wa sheria,” alisema.
Alisema ni ajabu
Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni wakati nchi
haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni,
Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa
kwenye Gazeti la Serikali.
“Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji Msigwa.
Alisema
licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai kuwa
hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba
wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na kuukosoa
utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.
“Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija bungeni mnakaa kimya.Huwa
tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja humu ndani,“ alisema
Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa ni
mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama kuomba mwongozo,
kupinga kauli ya mbunge huyo.
Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68
(7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka Mchungaji Msigwa athibitishe
kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri wanaopingana na uongozi wa
Serikali.
Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha
63 (1) (2), kinachomtaka mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo
ama apewe muda na kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na
Mchungaji Msigwa kuwasilisha ushahidi wao.
Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia?
Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge.
Msigwa:
Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio mwongozo
ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa. Ila
tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba.
Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana.
Akiendelea
na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi
yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba
hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na
kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
“Bunge ni
mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza kuminya na
kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya fedha za
Watanzania,” alisema.
“Serikali inayokandamiza uwazi ni
Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu. Mnasimama na kusema
mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha nini kuwaonyesha
Watanzania hiki mnachokifanya?”
Huku akiipongeza Serikali
iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mchungaji Msigwa
alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii watu kuzungumza na
kusema ukweli.
Post a Comment