0



pg 32 March 29UAMUZI wa kujitoa uliofanywa na timu ya Taifa ya Chad kwenye mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya  kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika

(AFCON) zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Gabon, umeondosha matumaini na ndoto za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kucheza fainali hizo.
Chad, katika mchezo wa kwanza uliochezwa

Alhamisi iliyopita Uwanja wa Omnisport Idriss Mahamat Ouya, mjini N’djamena, ilikubali kipigo cha bao 1-0.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Chad, Moctar Mahamoud, uamuzi huo wa kujitoa ulitokana na kukosa fedha za kutosha za kusafiri kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Taifa Stars, uliotarajiwa kuchezwa jana Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kutokana na kujitoa huko, mechi tatu za Chad za kundi G zimefutwa, hata matokeo yake ya michezo iliyopita hayatatambuliwa, hivyo msimamo wa kundi G utakuwa  unaongozwa na Misri, yenye alama 4, Nigeria alama 2 na Tanzania alama 1, timu zote zikiwa zimecheza michezo miwili.

Muathirika mkubwa wa kujitoa kwa Chad ni Taifa Stars,  ambayo ilikuwa na matumaini ya kufuzu kwa fainali hizo na ilionekana kuwa kwenye kiwango bora, ikiwa chini ya kocha mzawa, Charles Mkwasa na nahodha mpya, Mbwana Samatta, anayechezea timu ya K.R.C. Genk ya Ubelgiji.

Stars ilianza safari yake kwa kupoteza mchezo dhidi ya Misri kwa kufungwa mabao 3-0, baadaye kutoa sare dhidi ya Nigeria na kuifunga Chad bao 1-0.

Baada ya kufikisha alama 4, Stars ilikuwa na kila sababu ya kupambana na kuhakikisha inafanikiwa safari ya kuelekea Gabon, hata kwa nafasi ya pili ambayo ni ya upendeleo.

Lakini kwa maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Afrika ‘CAF’ yaliyofanywa Januari 15, 2015 yalidai kwamba kundi lolote litakalosalia na timu tatu kufuatia kujitoa kwa moja kwenye kundi hilo, kinara wa kundi hilo atafuzu moja kwa moja kwenye michuano hiyo.

Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo, kama timu itajitoa kwenye hatua ya makundi, matokeo yake yote yatafutwa.

Hivyo, kuna kila dalili kwamba Stars ikajikuta katika wakati mgumu wa kufuzu katika michuano hiyo kwa kuwa itabakiwa na alama moja, huku Misri ambayo ni kinara ina alama 4, Nigeria ikiwa ya pili kwa alama 2.

Timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’, ambao wamepangwa  kuchuana na Misri mjini Alexandria inabidi washinde alama zote ili kumaliza katika nafasi ya kwanza.

Wakati huo huo, Misri wanahitaji kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mchezo wa pili ili kuweza kujihakikishia safari ya Gabon mwakani.

Stars hata ikifunga michezo yote, bado haitakuwa na uhakika wa safari, kwani itakuwa na alama saba ambazo zitakuwa chache ukilinganisha na wapinzani.

Licha ya CAF kuitoza faini timu hiyo ya Chad dola za Kimarekani 20,000 na kuwapiga marufuku kushiriki  kwenye michuano  mwaka  2019, bado maumivu ya Watanzania hayatapona.

Matarajio ya Watanzania yalikuwa ni makubwa juu ya kufuzu kwa timu yao, kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kutandaza soka la kuvutia na wenye kuleta matokeo yoyote wanapokuwa uwanjani.

Zaidi ya yote, ndoto na matarajio hayo tayari yameshapotea kwenye vichwa vya Watanzania, hivyo kujikuta wakiendelea kusubiri huenda michuano ya mwaka 2019 Stars ikawa na bahati, lakini Chad imevuruga ndoto ya Watanzania.

Post a Comment

 
Top