0

Anna Kilango*
 Watumishi hewa wamponza

RAIS Dk. John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, baada ya kushika wadhifa huo kwa siku 22.

Mbali ya Kilango, pia Rais ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS), Abdul Rashid Dachi kutokana na kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa mkoa huo hauna watumishi hewa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli amechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa mkoa huo una watumishi hewa, tofauti na tamko la Kilango.

“Rais Magufuli ameeleza baada ya kupata taarifa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia  Aprili 10, 2016 imebaini kuwapo watumishi hewa 45 mkaoni Shinyanga, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya  za Ushetu na Shinyanga Vijijini,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia ilimnukuu Rais Magufuli akisema. “Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wamelipwa Sh milioni 339.9, nimejiuliza sana… na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwanini mkuu wa mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?,” alihoji Rais.

Taarifa hiyo, ilisema Rais Magufuli amewataka wakuu wa mikoa wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe katika orodha ya malipo ya mishahara, huku akiagiza timu iliyofanya uchunguzi

mkoani Shinyanga ifanye hivyo mikoa mingine ili kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
“Katikati ya Machi, mwaka huu, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote kusimamia kazi ya kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo mpaka Machi 31,watumishi hewa 5,507 walibanika.

“Kati ya Sh bilioni 583 ambazo Serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, kati ya hizo Sh bilioni 53 au 54, zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa,”ilisema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa Sh bilioni sita ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule, huku akitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo.

“Ameagiza fedha hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule mbalimbali nchini.

“Hundi kifani ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Rais na Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, ambaye amesema ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa Serikali kuhusu kubana matumizi.

“Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana matumizi kuwa, ni safari na mafunzo nje ya nchi, machapisho na ununuzi wa majarida, shajara, chakula, viburudisho, mtandao, malazi hotelini, matibabu ya wabunge na familia zao nje ya nchi, umeme, maji, simu na uendeshaji wa mitambo,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Uamuzi wa Rais Magufuli wa kutengua uteuzi wa Kilango, umetokana na kauli ya Kilango aliyoitoa mwishoni mwa Machi, mwaka huu  wakati akiwasilisha serikalini ripoti ya mkoa wake.

”Mkoa wa Shinyanga hauna mfanyakazi hewa hata mmoja kutokana na mpango waliojiwekea viongozi wa mkoa kwa watumishi waliopo kazini na kulipa mishahara kwa watumishi waliopo maeneo ya kazi pekee,”alisema Kilango.

Agoma kuzungumza
Gazeti hili lilimtafuta Kilango muda mfupi baada ya taarifa hiyo, lakini licha ya kuwa ofisini kwake, hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari.
Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, James Sibale aliwaambia waandishi wa habari waliofikia ofisini kwake, kuwa ‘bosi’ wake hawezi kuzungumza na waandishi wa habari kwa wakati huo.
“Mimi si msemaji wa ofisi, Kilango amesema sasa hivi hawezi kuzungumza na waandishi wa habari…mtapewa taarifa baadaye,”alisema Sibale.

KATIBU TAWALA
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi aliliambia MTANZANIA kuwa anakubaliana na uamuzi wa Rais Magufuli.

Alisema uamuzi uliofanywa na Rais ni sahihi kwa kuwa analenga kuboresha utendaji kazi serikalini.
“Nia ya Rais ni njema ili kuhakikisha nchi inakuwa haina watumishi hewa, sisi viongozi hatuna budi kuungana naye kuhakikisha hakuna mishahara hewa… tulitimiza wajibu wetu na hata watu

wakisoma taarifa yetu iliyowasilishwa na mkuu wa mkoa inaonyesha ni watumishi wepi ambao hawakustahili kuwa kwenye orodha ya walioondolewa katika ‘Payrol’.

“Sisi ni watendaji…tulikuwa tunapokea taarifa kutoka kwa watendaji wa Serikali wa ngazi ya chini, tunapokea na kutuma taarifa na kusimamia taarifa tulizopewa na wenzetu,”alisema Dachi.

SIKU 22 ofisini

Kilango alitambulishwa mkoani Shinyanga Machi 21, mwaka huu na baadaye akajitambulisha kwa wananchi katika mkutano wa hadhara Shinyanga Mjini uliofanyka Aprili 5 mwaka huu.

Katika mkutano huo, alisimikwa kuwa Chifu wa Kabila la Wasukuma na kupewa jina la “Mbula,” likiwa na maana ya mvua, likiwa ni jina la aliyekuwa mganga wa jadi maarufu wa 33 kati ya waganga wa jadi 54 nchini.

Kutenguliwa kwa Kilango kumekuja siku chache, baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi kumtahadharisha Kilango kufanya kazi kwa kufuata taratibu za utumishi wa umma.

MAONI
Baadhi ya wanasiasa wakongwe pamoja na wachambuzi mbalimbali waliozungumza na MTANZANIA, walieleza kusikitishwa na uamuzi  wa Rais Magufuli, wakisema ni wa kukurupa huku wengine wakipongeza hatua hiyo.

SUMAYE
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema Kilango hakuwa na hatia kiasi hicho kwa sababu bado hajaujua vizuri mkoa huo.

“Ukweli haiwezekani RC asimamie jambo hilo muda mfupi na hata akipewa miezi sita akakague watu hao ‘physically’ bado haitoshi.

“Kama aliletewa taarifa kuwa kuna watumishi hewa na yeye akasema hakuna…hapo kuna tatizo. Lakini ndio hivyo kila mtu na utawala wake, kumwajibisha mtu ambaye hata huo mkoa na ofisi hajaijua vizuri kwa kweli inasikitisha. Hii haijapata kutokea popote na si kitu cha kawaida,”alisema Sumaye.

PROF BAREGU

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu alisema kuna udhaifu mkubwa wa namna ya kuwapata wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu wakuu.

Profesa Baregu aliyepata kuwa Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema nafasi hizo zimekuwa zikitolewa kisiasa na ndio maana kumekuwapo na matatizo ya mara kwa mara kwa sababu viongozi hao hawajachekechwa.

“Hizi nafasi zilipaswa zipatikane kwa usaili yaani watu waombe au wapendekezwe halafu ndio wapewe nafasi hizo, lakini nafasi hizo zimekuwa zikitolewa kisiasa ndio maana haya yote yanatokea,”alisema msomi huyo.

Alisema kosa la pili alilolifanya Rais Magufuli, ni namna alivyotoa maagizo wakati kuna vyombo na taasisi zinazohusika katika uchunguzi, badala ya wakuu wa mikoa ambao hawana utaalamu wowote.
“Kwanini hakutaka kutumia vyombo vya ukaguzi na badala yake anawaambia wakuu wa mikoa? Tuna ofisi ya CAG na pale kuna watumishi wengi wa ukaguzi wangeenda wilayani na mikoani

kufanya uchunguzi lakini kuwaachia maRC ambao wengine ni walewale waliokuwepo katika baadhi ya mikoa…yaani ajikague mwenyewe halafu akuletee?

“RC hajui jinsi ya kuhesabu…katika hili Rais Magufuli amekurupuka kwa sababu kazi hiyo ilipaswa kufanywa na vyombo husika viandae taarifa kitaalamu. Sasa kwa sababu na yeye Kilango alipewa nafasi hii kisiasa naye anakubali na hana namna.

“Bado kazi ya ukaguzi kwa watumishi hewa haijafanyika ipasavyo, mpaka likifanyika kitaalamu ndio tutaelewa kwa sababu wapo ambao si hewa lakini wameunganishwa,”alisema Profesa Baregu.

WASIRA
 Mwanasiasa mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, Steven Wasira alisema alichokifanya Rais Magufuli ni kawaida kwa sababu kila kiongozi ana aina yake ya uongozi.
“Lakini hata wakati wa Nyerere (Mwalimu Julius) jambo kama hili lilitokea, kuna mtumishi mmoja simkumbuki kwa jina aliteuliwa na baadaye ikabainika hana sifa akatenguliwa ndani ya muda mfupi. Lakini hili ni jambo la Rais yeye ndiye ana mamlaka ya kuteua na kutengua,”alisema Wasira.

MSEKWA
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe na Spika mstaafu, Pius Msekwa alisema kila zama na kitabu chake na kwamba haiwezekani kuufananisha uongozi wa Magufuli na viongozi waliopita.
“Ni sahihi alichokifanya rais kwa sababu ndio ‘style’ yake ya uongozi na yeye ndio mwenye mamlaka ya kuteua na kutengua,”alisema.

Dk. Bisimba 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba alisema pamoja na kasi ya Rais Magufuli, lakini hajamtendea haki Kilango kwa sababu bado alikuwa mgeni katika mkoa huo.

“Huyu alikuwa ndio amefika tu na pengine watendaji ndio waliomdanganya sioni sababu ya yeye kuwajibishwa. Angepewa hata onyo kuwa awe mwangalifu zaidi.

“Na kwa mtazamo wa kijinsia tunaweza kudhani labda kwa sababu ni mwanamke kwani hata Rais anaweza kupewa taarifa za uongo na watu wa chini yake, lakini hatutamtoa madarakani,”alisema Dk. Bisimba.

PROF MPANGALA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaundence Mpangala alisema alichokifanya Rais Magufuli ni hatua za kinidhamu kwa watumishi wa serikali na kwamba wengine wajifunze.

  1. BANA
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema alichokifanya Rais itakuwa fundisho kwa viongozi waliopewa dhamana.

MACHALI

Aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, aliandika kupitia ukurasa wake wa facebook akimpongeza Rais Magufuli kwa hatua aliyoichukua.

“Kiukweli,  salute kwako ‘mr president’ kama kweli inavyoripotiwa mitandaoni kwamba umetengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mteule wako, tena wa juzi juzi tu, si jambo jepesi kwa kiongozi kumwadabisha mteule wake hapa Afrika na hasa Tanzania.

“Naanza kuiona Tanzania mpya na kuamini uliyowaasa wateule wako mbalimbali, tukio hilo litaongeza umakini na kuwafanya wakuu wa mikoa na wateule wengine serikalini kujenga tabia ya kufuatilia au kufanya uchunguzi au utafiti wa masuala yanayopaswa kutekelezwa na wao… keep it up mr president,” alisema Machali.

Taarifa hii, imeandaliwa na Elizabeth Hombo (Dar) ,Judith Nyange (Mwanza) na Kadama Malunde (Shinyanga)

Post a Comment

 
Top