Lengo lako la kutafuta ajira ni nini? Je? Ni kutafuta kulipwa mshahara? kutafuta mtaji? Au ni kwa ajili ya kujifunza mambo fulani kama sehemu ya maandalizi ya kufanya kitu fulani hapo baadae? Kimsingi maswali juu ya malengo ya kutafuta ajira ni mengi sana.
Lakini ukichunguza kwa undani unagundua kuwa lengo kuu la watu wengi kutafuta ajira ni kupata pesa kila mwezi na kuitumia. Lengo la kulipwa pesa kila mwezi likishakamilika, wengi hujaribu kutulia na kuridhika huku wakijaribu kubana matumizi ili kiasi kile kinachopatikana kila mwisho wa mwezi kiweze kutosha—japo kuwa huwa hakitoshi. Mshahara duniani kote huwa siyo zaidi ya asilimia 10% ya kile mtu anachozalisha.
Kwahiyo, mara nyingi tunajidanganya kila mara tunapodhani kuwa tutaweza kutimiza ndoto za maisha bora na endelevu kutokana na mshahara (ajira). Tukitaka kufaidi ajira yoyote, lazima tutambue kuwa ajira ni zaidi ya mshahara, uwe mdogo au mkubwa. Ajira yoyote ile inao uwezo wa kutupatia mambo mengine makubwa zaidi ya mshahara.
Ajabu na kweli ni kwamba, watu wengi kwenye ajira mbali na kupata mshahara, tunapata mambo mabaya ambayo kimsingi yamekuwa ni mwiba sugu kwa mafanikio yetu binafsi. Kwa walio wengi, ajira imekuwa ni sehemu ya kujenga tabia ambazo mwisho wake zinaangamiza badala ya kutujenga na kutuinua.
Mojawapo ya tabia mbaya ambazo watu huzijenga wawapo kwenye ajira zao ni pamoja na “kuchelewa kazini; kutegea kazi (uvivu); kulalamika; kupenda malipo ya papo kwa papo (kukosa uvumilivu), kila wakati kufanya vitu vinavyofanana na wenzako kazini (kukosa ubunifu); kupenda kufanyiwa kila kitu; kupenda kupongezwa n.k.
Wakati wote tunapojenga tabia za namna hii, tunadhani tuko salama na hatuoni madhara ya moja kwa moja kwetu, eti! kwasababu bosi wetu anaendelea kutulipa mshahara na marupurupu mengine. Ukweli ni kwamba, kwa tabia za namna hii, hatuko salama hata kidogo.
“Yatupasa kutambua kuwa, tabia unayoijenga ukiwa kwenye ajira ni mali yako na wala siyo mali ya mtu mwingine au shirika lililokuajiri”. Kwa maana nyingine ni kwamba wewe ndiye mmiliki wa tabia uliyoijenga ukiwa ndani ya ajira, iwe nzuri au mbaya ni yako tu.
Kila utakapokwenda utaambatana na tabia zako (mbaya na nzuri). Ikitokea ukahama shirika moja kwenda jingine, shirika unaloliacha linabaki salama, lakini endapo hutabadilika basi tabia zako zote unazihamishia kwenye shirika jipya—hili halitakuwa salama!
Hapa tunapata kujifunza kwamba, endapo tutaendekeza tabia mbaya tuwapo kwenye ajira, tusitegemee kubadilika pale tutakapoanza kufanya shughuli zetu binafsi. Kuna wakati ninaamini kwamba, Mungu anatuwezesha kupata ajira (kufanya kazi ya mtu mwingine), ili atuone na kutupima kabla ya kutupatia kazi (biashara) zetu wenyewe. Matarajio ni kwamba, kama unaweza kufanya vizuri kwenye ajira (kazi ambayo siyo yako), bila shaka utafanya kazi vizuri zaidi kwa kazi ambayo ni yako mwenyewe binafsi.
Umefika wakati sasa tutambue kuwa nafasi za ajira tulizonazo au tunazotarajia kupata, ni awamu ya pili ya SHULE. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wengi tunapata ajira baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya shule, mfano: “shule ya msingi, sekondari, chuo” n.k. Kama ilivyo kwa awamu ya kwanza ya shule, awamu ya pili— “ajira”, inakutaka kusoma na kumaliza ndani ya miaka 5—10 kutegemea na kile ulichoajiriwa kufanya.
Ikiwa umejipanga vizuri, miaka 5—10 inakutosha wewe kuanza maisha ya kijiongoza mwenyewe. Ukiwa umeajiriwa huwezi kusema kuwa unajiongoza mwenyewe. Tunasisitiza maisha ya kujiongoza mwenyewe, kwasababu ukiwa bado kwenye ajira ni lazima kufanya kazi zile ambazo unaelekezwa na mmiliki wa ajira yako na siyo kwa mujibu wa unavyofikiri wewe binafsi.
Ni vizuri pale tunapofanya maamuzi ya kuingia kwenye ajira, tupange na kuamua ni muda gani tutatumikia ajira. Muda au miaka tutakayoipanga kukaa ndani ya ajira, lazima iwe inatosha na ituwezeshe kuwa tumekomaa, tumefuzu na kupata sehemu kubwa ya yale yote ambayo yanatuwezesha kuanza kujiongoza au kumiliki kazi.
Unapoona mtu ameamua kutumikia ajira yake kwa miaka mingi, basi ujue kuwa mtu huyo bado haichukulii ajira kama SHULE. Kwa mtu ambaye yeye haichukulii ajira yake kama shule, kwake yeye ajira ndiyo machimbo ya kudumu ya pesa, japo kiasi kipatikanacho huwa hakitoshi kuweza kuleta utajiri au kukutoa kwenye umaskini.
Kwa maneno mengine ni kwamba pesa tunayopata kama mshahara huwa ni kidogo na inasaidia tu kuvumilia umaskini na wala sikututoa kwenye umaskini. Kwahiyo, lazima ujitahidi kusoma kwa bidii na maarifa na umalize shule yako ya awamu ya pili (ajira), ili hatimaye uweze kustaafu mapema na haraka iwezekanavyo.
Usifikiri kustaafu ajira ni lazima ufikishe miaka 60—hapana! Kustaafu ni pale unapoacha kutumwa kazi; kupewa maelekezo ya nini cha kufanya, muda gani ukifanye, na ukifanye kwa manufaa ya nani, pia kupata uwezo wa kujichagulia watu wa kufanyanao kazi n.k.
Wito wangu kwa wote tulioajiriwa ni kwamba lazima tujitahidi kuwa na mtazamo chanya juu ya ajira zetu. Tuendelee kutumia vizuri muda wetu wote ambao tuko ndani ya ajira katika kujenga tabia za mafanikio.
Kwa kufanya hivyo itatufanya kutoa matokeo makubwa kwa taasisi ambazo zimetuajiri, LAKINI pia tutapata fursa ya kujijenga sisi binafsi katika kila nyanja ya maisha yetu. Lazima tuhakikishe tunafanya kazi kama vile ni za kwetu na kikubwa zaidi, tuendelee kuziona na kuzichukulia ajira kama DARASA kama siyo SHULE.
Post a Comment