0




Benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha wake mkuu, George Lwandamina, limeweka bayana kuwa sasa linaelekeza nguvu zake kuhakikisha linatwaa ubingwa wa ligi kwa kuwa tayari limeshakosa makombe manne.


Yanga wikiendi iliyopita ilivuliwa ubingwa wa kombe la Shirikisho baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mbao, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ukiondoa ubingwa huo wa FA, pia Yanga wameshakosa mataji zaidi ya manne waliyokuwa wakishindania msimu huu ambayo ni Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi ya Mabingwa na Ngao ya Jamii.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema sasa wanaelekeza nguvu zao kuhakikisha wanashinda kwenye mechi zao tano zilizobakia ambapo wana matumaini ya kushinda zote Kwa kuwa michuano hiyo ndiyo pekee wanayoitolea macho kwa sasa.

“Hatutaki kuona tunatoka kapa msimu huu baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wowote ule kwenye zaidi ya mashindano matano ambayo tulikuwa tunashindania kwa msimu huu na sasa tunaelekeza nguvu zetu katika ligi.

“Tunaamini kwamba tuna uwezo mkubwa wa kushinda mechi zetu zote kwani zenyewe ndiyo zipo kichwani mwetu na hilo ndilo tumaini pekee lililobaki la kuchukua ubingwa na naamini kwamba kama tukijitoa kwa kushirikiana basi hakuna ambacho kitatufanya tukose taji hilo,” alisema Mwambusi.

Yanga kwa sasa imebakiza mechi tano dhidi ya Prisons, Mbeya City, Toto Africans, Kagera Sugar na Mbao, ambapo sasa wana pointi 56, katika nafasi ya pili na wakishinda mechi zote hizo watafikisha pointi 71 ambazo zitakuwa tatu mbele ya Simba ambao watamaliza na 68 kama wakishinda mechi zao zote tatu.     

Post a Comment

 
Top