0



UTAFITI wa viashiria na matokeo ya Ukimwi wa mwaka 2016 ambao unahusisha upimaji wa ugonjwa huo kaya kwa kaya kwa Mkoa wa Dar es Salaam, utaanza kufanyika Mei mwaka huu, ambapo jumla ya kata 31 kutoka wilaya tatu za mkoa huo ndizo zitakazoshiriki.

Utafiti huo pia utahusisha ukusanyaji wa taarifa zisizohusu maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), kiwango cha VVU mwilini na kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo, wastani wa maambukizi kwa watu wa rika zote na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4).

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda wakati wa uzinduzi wa utafiti huo wa mwaka 2016/17 na kusema kuwa wakati wa utafiti huo, baadhi ya vipimo ambavyo wanakaya watapimwa, vitatolewa majibu papo hapo.

Utafiti huo umeanza kufanyika Oktoba mwaka jana na unatarajia kukamilika Julai mwaka huu ambao unashirikisha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Shirika la ICAP la Chuo Kikuu cha Columbia na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).

Aidha, alisema utafiti huo ni wa nne kufanyika nchini, unaoangalia masuala ya afya ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003/2004, wa pili ulifanyika 2007/2008 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011/12.

Alisema katika tafiti hizo zilikuwa zikiwahusisha wananchi wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 tofauti na utafiti huo ambao kwa mara ya kwanza utawahusisha wananchi wa rika zote katika kaya zilizochaguliwa.

Mjema alisema utafiti huo utaangazia viashiria vya usugu wa dawa, kiwango cha maambukizo ya kaswende na homa ya ini kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi. Sambamba na hayo, utafiti huo pia utakusanya taarifa za upatikanaji na utumiaji wa huduma zitolewazo katika kudhibiti maambukizi ya VVU na Ukimwi na viashiria vya tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU.

Post a Comment

 
Top