0



Utangulizi
Wiki na miezi iliyopita kumekuwepo na mijadala mizito ya kisiasa na kitaifa juu ya masuala ya upungufu wa chakula Tanzania.

Taaarifa za upungufu wa chakula mwanzoni zilikataliwa na viongozi wa juu wa serikali lakini baadae walikiri kuwepo kwa upungufu wa chakula nchini. Mwishoni mwa mwezi Januari 2017, Waziri wa Chakula, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba aliliambia bunge kwamba utafiti uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau kadhaa 1 , umegundua kwamba Wilaya 55 (kati 169 za Tanzania Bara na Visiwani) zilikumbwa na njaa, na tani “35,491 za nafaka zinahitajika kusambazwa kati ya mwezi wa pili na wa nne mwaka 2017 ili kukabiliana na upungufu huo uliowakumba watu 1,186,028” 2 katika Wilaya hizo.

Waziri Tizeba alilalamikia kupanda kwa bei za vyakula katika maeneo mengi na alisema hii inasababishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu wanaotumia mianya ya njaa, pamoja na uhitaji mkubwa wa mahindi katika nchi jirani. Matokeo yake ni kusababisha bei za ndani kupanda. Aliongeza kwamba “Serikali imeanza kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo ambayo ni pamoja na kutoa chakula kutoka hifadhi za taifa na kuuza kwa bei nafuu katika maeneo yaliyo athirika.”

Sintofahamu hii juu ya hali ya chakula nchini imetokea katika kipindi ambacho uchumi wa Tanzania umekua kwa kasi nzuri ya asilima saba kwa mwaka. Lakini ukuaji huu haujafanikiwa kuondoa umasikini kwa kiwango kilichotarajiwa na wengi. Asilimia 68 ya wananchi bado wanaishi chini ya kiwango cha umasikini cha $1.25 kwa siku 3 . Pamoja na hayo kiwango cha udumavu kimeendelea kuonekana kwa watoto chini ya miaka 5 4 , ukiachilia mbali mafanikio madogo yaliyopatikana katika miaka ya karibuni kwenye utoaji wa lishe nchini. Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Tanzania (NBS) na UNICEF wanakadiria kuwa robo tatu ya watoto wote wa Tanzania asilimia 74) wanaishi kwenye umasikini mkubwa 5 .

Muhtasari huu unawasilisha takwimu za maoni ya wananchi na uzoefu wao katika hali ya upungufu wa chakula na sababu zake. Ni kaya ngapi na jamii zipi ambazo zimekumbwa na njaa? Ni vyakula vipi vilivyo adimu kupatikana? Na ni kwa namna gani bei za vyakula zimepanda ikilinganishwa na miezi michache iliyopita?

Takwimu za muhtasari huu zimetokana na utafiti wa Twaweza wa Sauti za Wananchi. Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi mkubwa unaotumia simu za mkononi. Uwakilishi huu ni wa Tanzania bara. Maelezo zaidi juu ya utafiti huu yanapatikana katika tovuti ya www.twaweza.or.tz/sauti. Takwimu za muhtasari huu zilikusanywa katika awamu ya pili ya kundi la pili la Sauti za Wananchi.

  1. Wahojiwa 1,800, awamu ya 13 ya kupigiwa simu kwa kundi hili la wahojiwa, kati ya tarehe 14 - 26 Septemba 2016.
  2. Wahojiwa 1,610, awamu ya 16 ya kupigiwa simu kwa kundi hili la wahojiwa, kati ya tarehe 9 - 15 Februari 2017.
Matokeo makuu ni:
  • Kaya nane kati ya kumi (asilimia 80) zimeripoti kwamba kipato chao hakikidhi mahitaji yao ya kila siku.
  • Kaya nane kati ya kumi (asilimia 79) huweka akiba ya chakula kwa ajili ya kijitosheleza ifikapo vipindi vya njaa.
  • Wahojiwa wengi wa Sauti za Wananchi (asilimia 78) wanaripoti upungufu wa chakula katika maeneno wanayoishi
  • Bei ya mahindi imepanda mara mbili katika kipindi cha miaka miwili na kusababisha ongezeko la bei katika bidhaa.
  • Kaya saba kati ya kumi (asilimia 69) zilihofia kukumbwa na njaa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
  • Hali ya upungufu wa chakula imekua mbaya zaidi katika kipindi cha mwezi wa Septemba mwaka 2016 hadi Februari, 2017.
Mambo nane muhimu kuhusu hali ya chakula Tanzania

Jambo la 1: Kaya nane kati ya kumi zimeripoti kwamba kipato chao hakikidhi mahitaji yao ya kila siku.

Mwezi Septemba mwaka 2016 kaya nane kati ya kumi (asilimia 80) ziliripoti kuwa na kipato kisichokidhi mahitaji yao ya kila siku. Takwimu hizi zinatofautiana kidogo katika kaya za mijini na zile za vijijini au kati ya kaya masikini na kaya tajiri.

Kielelezo cha 1: Je kipato kinachopatikana katika kaya kinatosha kukidhi mahitaji ya kila siku ya nyumbani?

1.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)

Kaya tano kati ya sita (asilimia 85) zinasema kwamba kipato kinapopungua wanalazimika kubana matumizi. Idadi ndogo inasema watakopa bidhaa (asilimia 6) na wengine huripoti kwamba watakopa fedha zaidi (asilimia 2).

Walipoulizwa kukadiria ni kiasi gani cha fedha kingetosha kwa ajili ya mahitaji ya kaya ya kila siku, wastani wa makadirio yote yalikua shilingi 1,777 kwa mwanakaya au shilingi 10,662 kwa kila kaya 6 . Kwa mwanakaya anaeishi mjini makadirio yalikuwa juu kidogo (shilingi 2,247) kuliko kijijini (shilingi 1,579). Makadirio pia yalikuwa makubwa zaidi kutoka kwenye kaya zenye uwezo (asilimia 20 ya waliokuwa na utajiri wa juu sana - Shilingi 2,304) ukilinganisha na kaya masikini (asilimia 20 ya waliokuwa na umasikini wa chini kabisa - Shilingi 1,577).

Jambo la 2: Wananchi tisa kati ya kumi wanaona ni jukumu lao wenyewe kuhakikisha wana fedha za kutosha za kukidhi mahitaji ya kaya zao

Idadi kubwa ya wananchi (asilimia 87) wanasema iwapo watakosa fedha za kukidhi mahitaji ya chakula kwa ajili ya familia zao, hawatarajii watu wengine kulichukua jukumu hilo. Hata hivyo, asilimia 17 ya wanawake na asilimia 9 ya wanaume wangetarajia msaada kutoka nje.

Kielelezo 2: Iwapo ungekuwa huna pesa za kukidhi mahitaji ya chakula kwa ajili ya familia yako pamoja na kaya yako, je unadhani ni jukumu la mtu kukusaidia au ni jukumu lako mwenyewe?

2.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)

Miongoni mwa wale wananchi wachache (asilima 13) wanaofikiri kwamba ni jukumu la mtu mwingine kuwasaidia katika hali hiyo, nusu yao (asilimia 49) wamesema ni wajibu wa serikali kutoa msaada. Idadi ndogo wamesema ni wajibu wa wanandugu (asilimia 36) au marafiki na majirani (asilimia 7).

Jambo la 3: Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kaya moja kati ya nne imepokea fao, faida au pesa kutoka kwenye miradi ya serikali

Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kuanzia mwezi wa tisa 2015 mpaka mwezi wa tisa 2016, asilimia 25 ya kaya zimepokea fao, faida au pesa kutoka katika vyanzo vifuatavyo:
  • Sare za shule, kadi ya matibabu, chakula na kadhalika kutoka kwenye Mpango wa Watoto Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu
  • Nafaka za bure kutoka kwa viongozi wa kijiji na Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula (NFRA)
  • Chakula cha shule kinachotolewa na Mpango wa Chakula Shuleni
  • Kazi za jamii zinazotolewa na Tanzania Social Action Fund (TASAF)
  • Pesa zinazotolewa na TASAF kwa ajili ya kunusuru kaya masikini
  • Vocha za mbolea/mbegu zinazotolewa na Mpango wa Taifa wa Ruzuku na Kilimo
  • Malipo ya mafao kutoka Mfuko wa Pensheni wa Taifa (NSSF)
  • Malipo ya mafao kutoka Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF)

Kielelezo 3: Mafao au faida zilizopokelewa ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita
(Asilimia ya kaya zinazopokea mafao haya)
Screenshot from 2017-03-01 12:03:22.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)

Jambo la 4: Kaya nane kati ya kumi huweka akiba ya chakula

Kaya nane kati ya kumi (asilimia 79) zimeripoti kwamba wana hifadhi chakula kwa ajili ya dharura au kuepukana na njaa. Wananchi wengi zaidi wa vijijini huhifadhi (asilimia 87) kuliko wa mijini (asilimia 61) na kaya masikini huhifadhi kuliko kaya tajiri. Uhifadhi wa chakula pia uko juu kwa kaya ambazo hutegemea zaidi kilimo kama sehemu kubwa ya kipato chao (asilimia 92) kuliko kaya ambazo hutegemea vyanzo vingine vya mapato kama vile biashara au ajira (asilimia 49).

Kielelezo cha 4: Je, kaya yako huhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati wa dharura au njaa?
(Asilimia iliyojibu ndiyo)
4.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 16 (Februari 2017)
Jambo la 5: Wahojiwa wengi wa Sauti za Wananchi (asilimia 78) wanaripoti upungufu wa chakula katika maeneo wanayoishi.

Asilimia 78 ya wahojiwa wa Sauti za Wananchi waliripoti kuwa upungufu wa chakula ulikuwepo katika maeneno wanayoishi. Hali hii ilijitokeza zaidi kati maeneo ya vijijini (asilimia 84 wakisema kuna upungufu wa chakula) kuliko mijini (asilimia 64 wakisema hivyo).

Kielelezo cha 5: Je eneo unapoishi lina upungufu wa chakula?
(Asilimia iliyojibu ndiyo)
5.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 16 (Februari 2017)

Jambo la 6: Bei ya mahindi imepanda sana katika kipindi cha miaka miwili.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania 7 bei ya mahindi imepanda kutoka shilingi 400 kwa kilo mwanzoni mwa mwaka 2015 mpaka shilingi 852 kwa kilo kufika mwezi Desemba 2016. Bei ya mahindi imepanda kwa kiwango cha juu sana ikilinganishwa na kiwango cha mfumuko wa bei wa kipindi hiki, Pamoja na mfumuko wa bei, hii inawasilisha kuongezeka mara mbili zaidi kwa bei ya mahindi katika kipindi hiki 8 .

Wahojiwa wa Sauti za Wananchi wameripoti kuwa bei hizi zimeongezeka zaidi baada ya Benki ya Tanzania kutoa takwimu zake hadi kufikia 1,253 kwa kilo moja. Hata hivyo, ni lazima ifahamike pia kwamba takwimu hizi zimejikita katika bei zilizoripotiwa kwenye masoko ya ndani, wakati takwimu za Benki ya Tanzania zimejikita katika bei halisi za wasambazaji wa jumla.

Kielelezo cha 6: Bei ya mahindi kwa kilo
6.png
Chanzo cha takwimu: Ripoti za Benki Kuu ya Tanzania (Januari 2015 – 2017) Sauti za Wananchi - Awamu ya 16 (Februari 2017)

Kaya mbili kati ya tatu (asilimia 68) zimeripoti upungufu wa mahindi katika maeneo yao kuliko upungufu wa mchele ama maharage (asilimia 4). Uchambuzi wa takwimu hizo za bei toka Benki kuu ya Tanzania zinaonesha kwamba bei za mchele na maharage hazijapanda sana katika kipindi hicho hicho cha miaka miwili tangu mwanzoni mwa 2015. (haijaoneshwa kwenye kielelezo.)

Jambo la 7: Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kaya saba kati ya kumi zimepata hofu ya kupungukiwa na chakula.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita (Novemba 2016 mpaka Februari 2017) kaya saba kati ya kumi (asilimia 69) zimepata hofu ya kupungukiwa na chakula.
Matokeo pia yanaonesha kwamba:
  • Asilimia 50 ya wananchi wamelazimika kupunguza idadi ya milo kutokana na kukosa fedha au rasilimali zingine.
  • Asilimia 51 wamepungukiwa na chakula au.
  • Asilimia 50 wamelazimika kushinda na njaa kabisa.
Katika hali zote hizi, kiwango cha upungufu wa chakula ni mkubwa katika sehemu za vijijini
kuliko mjini.

Kielelezo cha 7: Ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita ....
(Asilimia iliyojibu ndiyo)
7.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu 16 (Februari 2017)

Jambo la 8: Hofu ya kupungukiwa na chakula imeongezeka sana kati ya Septemba 2016 na Februari, 2017

Mwezi Septemba mwaka 2016, asilimia 45 waliripoti hofu ya kupungukiwa na chakula. Hata hivyo, ilipofika Februari 2017, idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia asilimia 65 wakiripoti hofu ya kupungukiwa na chakula. Ongezeko hili katika kipindi cha miezi mitano ni kubwa.

Mwezi Septemba 2016, kaya nne kati ya kumi (asilimia 43) ziliripoti kuwa, katika kipindi cha miezi kumi na mbili ya awali, zilikumbwa na upungufu wa chakula. Miezi mitano baadae, (Februari 2017) kaya tano kati ya kumi (asilimia 51) ziliripoti kukumbwa na upungufu mkubwa wa chakula kati ya Novemba 2016 na Februari 2017.

Jedwali la 8: Upungufu wa chakula mwezi Septemba 2016 na Februari 2017 (Asilimia iliyojibu ndiyo)
Je, ndani ya siku saba zilizopita, je ulipata hofu yoyote kwamba kaya yako haitokuwa na chakula cha kutosha?

8.png
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016) Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 16 (Februari 2017)

Pamoja na hayo, katika kipindi cha miezi sita kabla ya Septemba 2016, kaya moja kati ya tano (asilimia 21) iliripoti kwamba mtu mmoja ndani kaya

Post a Comment

 
Top