0
SeeBait
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameibuka na kueleza kushangazwa na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wabunge wa CCM waliotaka kwenda kumwona gerezani walikuwa wasaliti.

Lema alisema anatarajia Spika wa Bunge, Job Ndugai, atatoa msimamo juu ya kauli ya kiongozi huyo wa nchi.

Kauli hiyo ya Lema imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuripotiwa na chombo kimoja cha habari  kwamba alishangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembelea Lema gerezani.

Katika mkutano wake na wabunge hao juzi uliofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema amekuwa akielezwa kuwa kamati hiyo ilikuwa imepanga safari za kutaka kwenda kumwona Lema alipokuwa gerezani jambo ambalo alilifananisha ni sawa na usaliti kwa chama chake.

Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Lema alisema kitendo cha wabunge hao kutaka kumtembelea si usaliti bali ni upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.

Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

“Mheshimiwa Rais Magufuli nakusalimu. Nimetoka gerezani hivi karibuni ambako nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana kwa dhamana iliyokuwa wazi.

“Nimeona kwenye vyombo vya habari leo kwamba wale wabunge waliokuwa wanataka kunisalimia nilipokuwa magereza ni wasaliti wa chama cha CCM.

“Mheshimiwa Rais wengi walinisalimia wakiwemo wachungaji, masheikh, wabunge na viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.

“Mheshimiwa  Rais nimeogopa sana kwa kauli hii, je Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya,” alisema Lema.

Mbunge huyo alisema dhambi hiyo ikikomaa ni wazi kwamba lugha za kidini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa.

Alisema ni muhimu sasa wakajenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli wanapenda masikini na wanyonge.

“Nawaomba wabunge wenzangu walionijali wakati niko gerezani wasijisikie vibaya kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika maisha yangu ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa neon juu ya kauli hii ya Rais.

“Mheshimiwa Rais wakati wa msiba wa Christina Lissu dada yake na Tundu Lissu, nilikuona katika msiba ule wewe na mama yetu mke wako, je wewe ulikuwa unasaliti chama chako?

“Meshimiwa Rais neno la Mungu linasema wapendeni maadui zenu, waombeni wanaowadhi, wabarikini wanaowaonea kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za Mwenyezi Mungu,”alisema Lema.

Mbunge huyo alisema pamoja na hali hiyo ya kuzuiwa lakini aliwashukuru wabunge wa CCM kwa kwenda kumjulia hali, akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka gerezani.

“Sina la kusema katika hili kama Rais alikuwa anajua hawakuja kuniona gerezani lakini niwashukuru wabunge wa CCM wote waliokuja kunijulia hali nyumbani. Sisi kama nchi tunatakiwa kuwa na umoja badala ya kuanza kubaguana kwa itikadi zetu za vyama.

“Mdogo wangu wa kike amepata mchumba lakini familia ya huyo mchumba wake inatokana na CCM je tuvunje vikao vya harusi kwa sababu ya tofauti ya vyama?

“Jibu ni hapana sisi ni Watanzania ni lazima tuishi kwa kupenda na kwa umoja kama ambavyo utamaduni wetu unatutaka na si vinginevyo,” alisema.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma nje ya viwanja vya Bunge na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 4 mwaka jana akikabiliwa na kesi mbili namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 440, anadaiwa kati ya Oktoba 22 mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii kwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.

Katika kesi ya pili namba 441, alidaiwa kwamba, Oktoba 23, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema  alitoa maneno kuwa:

“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, nimeota  Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake,”.

Februari 27,  mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania ilifuta rufaa mbili za Jamhuri dhidi ya Lema baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama  hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na rufaa, hivyo kuiomba mahakama kuzifuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana ya mbunge huyo.

Post a Comment

 
Top