0




 DAR ES SALAAM: Hapatoshi na joto la ugomvi linazidi kupanda kila kukicha kufuatia mama wa mwigizaji Wema Isaac Sepetu, Mariam Sepetu kuingia kwenye mgogoro mzito na Mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’. Wawili hao wameingia kwenye mgogoro huo baada ya Steve kumtuhumu mama Wema kuvujisha mazungumzo yao ya siri yaliyoshusha tuhuma nyingi kwa viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo mawaziri.

MUVI ILIVYOANZA
Baada ya mazungumzo hayo ya siri kuvuja Alhamisi iliyopita, tathmini za wachangiaji mbalimbali mitandaoni, zilimmwagia lawama mama Wema kwa kuhusika na kusambaa kwa sauti hiyo kwani asilimia kubwa ya mazungumzo yaliyosikika katika ‘clip’ ya sauti hiyo, yalikuwa yakimuaibisha na kumfanya aonekane mmbeya mbele ya jamii hivyo isingekuwa rahisi Steve kuyavujisha.

STEVE NAYE ANENA
Siku hiyohiyo, Steve alizungumza na gazeti dugu na hili, Risasi Jumamosi  ambapo alieleza kwa kifupi kuwa, mama Wema amehusika katika kuvujisha sauti hiyo ili amharibie maisha yake kwani mazungumzo yake yatakuwa yamewachafua mawaziri hao kwa kitendo cha kuwahusisha na suala zima la kumtetea Wema bungeni katika msala wake wa madawa ya kulevya.

WAFIKA PABAYA
Kikizungumza na mwanahabari wetu, chanzo makini ambacho kipo karibu na Steve, kilisema kuwa kitendo cha kuaminika kwamba mama Wema ndiye aliyevujisha sauti hiyo, kilimsikitisha Steve ambapo aliapa kula naye sahani moja kwani bimkubwa huyo alionekana kudhamiria kumharibia maisha. “Steve alikasirika sana. Aliona kabisa mama Wema amemchezea mchezo kwani alipofanya tathmini ya harakaharaka, aligundua kabisa mama Wema alimpigia simu na kumuingiza kwenye mtego makusudi ili yeye aweze kuingia kingi.

“Ndiyo maana ukisikiliza ile sauti, mama Wema alikuwa anamkazania katika eneo lile Odemba aangua kilio Dar muhimu la kumtuhumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda) ndipo Steve naye akawa anajaa tu bila kujua dhamira ya mama Wema,” kilisema chanzo hicho.

STEVE AJIKOKI

Chanzo hicho kilizidi kuweka bayana kuwa, kitendo hicho cha Steve kuamini mama Wema amemwaga mboga, naye alianza kukusanya data zake ili amwage ugali maana ameona hakuna sababu ya kumtendea haki mtu ambaye amedhamiria kumharibia maisha. “Wewe si unajua Steve na mama Wema wemeshafanya mengi, walikuwa karibu, sasa Steve naye hawezi kukubali, atakuja na bonge moja la bomu ambalo akililipua, mama Wema hatakaa asahau maishani mwake,” kilisema chanzo.

MAMA WEMA HAJALI

Wakati chanzo hicho kikieleza kwamba Steve amejikoki kulipuka na jambo, Ijumaa iliyopita, mama Wema na mwanaye waliitisha mkutano wa vyombo vya habari nyumbani kwake na kueleza kwamba wameamua kuingia vitani kupigania ‘haki’ na alipoulizwa kuhusu kuvujisha sauti yake na Steve, hakuonekana kujali.

“Mimi sijashika simu, halafu kwanza Steve ni mwanangu tu…,” alisikika mama Wema ambaye pia alitumia mkutano huo na mwanaye kutangaza kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

WEMA NAYE ALIKINUKISHA

Katika mkutano huo, Wema alisema anatambua kuwa ana kesi lakini kilichomfanya afanye uamuzi huo ni kupigania haki kwa kile alichosema hata kama alikuwa mtuhumiwa, hakupaswa kuchukuliwa kama alivyochukuliwa wakati yeye ana heshima kwenye jamii na alikipigania Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Wema alienda mbali zaidi na kusema, yeye pamoja na wasanii wenzake, wanakidai chama hicho tawala na kwamba licha ya kuongoza dola, hakijamtendea haki hata kama alikuwa mtuhumiwa.


STEVE NAYE ATEMA CHECHE
Juzi Jumamosi, Steve naye aliandaa mkutano wa waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine ya ufafanuzi wa yale yaliyosikika katika ‘audio’ yake na mama Wema, alitumia mkutano huo kupinga mambo aliyoyazungumza Wema aliyoona ni ya uongo likiwemo la kudai hawakulipwa katika kampeni.

“Hakuna msanii ambaye anakidai chama katika Timu ya Mama Ongea na Mwanao ambayo mimi nilikuwa mwenyekiti na Wema akiwa makamu mwenyekiti, sijui labda timu nyingine. Kwanza jamani, ifike mahali tuseme ukweli. Wema ninaweza kusema ndiye msanii pekee ambaye alilipwa hela nyingi kuliko wasanii wengine wote,” alisema Steve katika mkutano huo.

MAMA WEMA KUBURUZWA MAHAKAMANI?
Hata hivyo, chanzo kilicho karibu na Steve, kimeeleza kuwa huenda Steve akamfungulia mashitaka mama Wema kwani Sheria ya Makosa ya Mtandao inamruhusu. “Sheria ya makosa ya mtandao imemkalia vibaya kweli mama Wema kwa sababu inaonesha dhahiri yeye ndiye kahusika kumchafua. Steve nilivyomuona, siku si nyingi atamburuza mahakamani,” kilisema chanzo hicho.

MDAU ANENA
Mdau mkubwa wa sinema za Kibongo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema suala hilo anavyoliangalia limefika pabaya kwani sasa kila upande unajipanga kumtupia mwenzake mashambulizi na ukizingatia suala limeshakuwa la kivyama sasa.

“Wewe si unajua Wema na mama’ke wamehamia Chadema, watafanya kila linalowezekana ‘kumpiga’ Steve aonekane hafai na Steve naye hatakubali, ameandaa mashambulizi ya kila namna kuhakikisha anawabomoa Wema na mama’ke hivyo sasa hivi usitegemee tena Steve akawa na uhusiano mzuri na familia ya Wema,” alisema mdau huyo.

WALIKOTOKA!
Kabla ya kufikia hapo, Wema na Steve walikuwa marafiki wakubwa walioshibana hadi kufikia hatua ya kuwa kama ndugu kwani familia ya mama Wema iliamini Steve ni kama mtoto wao. Steve na Wema wameshirikiana katika dili nyingi mjini zilizowafanya waingize fedha pamoja serikalini na hata sekta binafsi lakini sasa wamegeuka chui na paka.
Tupe Maoni Yako Hapa Chini ( Matusi Hapana )

Post a Comment

 
Top