Kusambaa kwa sauti iliyorekodiwa mazungumzo ya mwigizaji Steven Mengele
‘Steve Nyerere’ na mama wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Mariam
Sepetu halijafutika, mengine yamefumka kwani baadhi ya wabunge
waliotajwa kwenye sauti hiyo wamelimpua Steve. Mbali na wabunge kutajwa
katika sauti hiyo iliyosambaa wiki iliyokatika, wasanii pia walitajwa
ambao ni Khaleed Mohamed ‘TID’, Romeo George ‘Rommy Jones’ na Ahmed
Hashim ‘Petit Man’.
Kwa upande wa wabunge ni Goodluck Millinga (CCM-Ulanga), Ahmed Shabiby
(CCM-Gairo), Joseph Musukuma (CCMGeita Vijijini), Freeman Mbowe
(Chadema-Hai) na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo, Kigoma Mjini).
Steve pia aliwataja mawaziri wawili. Steve alisikika akiwataja wabunge
hao akimwambia mama Wema kuwa, aliwafuata bungeni mjini Dodoma, Februari
6, mwaka huu ili wamsaidie bintiye aliposhakiliwa kwenye Kituo Kikuu
cha Polisi Dar ‘Sentro’ kwa madai ya kujihusisha na matumizi ya madawa
ya kulevya, ikiwemo kukutwa na bangi.
STEVE AOMBA RADHI WOTE
Hata hivyo, baada ya sauti hiyo kusambaa mitandaoni Februari 23, mwaka
huu na kuwa gumzo, Jumamosi iliyopita, Steve alifanya mkutano na
waandishi wa habari katika Jengo la Millennium Tower, Kijitonyama na
kuwaomba radhi wote aliowataja huku akikiri sauti ni yake na kwamba,
hakuzungumza nao kama ‘alivyomwongopea’ mama Wema bali aliwataja katika
hali ya kudumisha ukaribu wake na familia ya mama huyo.
UWAZI NA WABUNGE
Baada ya mkutano huo, Uwazi liliwatafuta wabunge hao, kasoro Mbowe
hakupokea simu, na waliopatikana walikuwa na haya ya kusema: SHABIBY:
“Steve Nyerere namfahamu. Lakini sina ukaribu naye. Niliwahi kukutana
naye muda mrefu kwenye hoteli yangu ya Moleno, Dodoma.
“Nakumbuka alikuja na mwanamuziki Ray C (Rehema Chalamila), lakini baada
ya hapo sijawahi kuonana naye popote maana hata baada ya kukutana naye
sikuwahi kuwasiliana naye. “Kuhusu kunihusisha mimi katika sakata la
Wema, yale mazungumzo nimeyasikia vizuri. Si kweli alichokisema eti
alikuja kukutana na Musukuma kwenye hoteli yangu na mimi nikiwepo. Ni
uongo mtupu.
“Sijaonana na Steve Nyerere katika siku za hivi karibuni na sijazungumza
naye lolote lile hata kwa njia ya simu,” alisema Shabiby.
MILLI NGA: “Ninafahamu kila kitu kinachoendelea, maana Steve Nyerere ni
mtu ambaye tunakutana mara kwa mara, ukizingatia ni kada mwenzangu
kwenye Chama Cha Mapinduzi. Kuhusu yeye kunishawishi mimi kumtetea Wema
bungeni, jambo kama hilo halipo maana sikuwahi kukutana naye kabla ya
mimi kuzungumza bungeni. “Ila baada ya bunge, jioni nilikutana naye,
akaniambia kuwa, nilichokiongea ni kama nilitazama kilichokuwa moyoni
mwake.
Hata hivyo, nimemsamehe maana ameomba radhi kwenye mkutano na waandishi wa habari!”
ZITTO: “Mimi siwezi kusemea jambo hilo maana mimi kwangu halina maana yoyote.”
MUSUKUMA: “Nisikilize vizuri mwandishi, mimi Steve Nyerere hana mchango
wowote kwenye maisha yangu. Mimi ni Mbunge wa Geita Vijijini na sifanyi
kazi yangu ya ubunge kwa kushawishiwa na mtu. “Steve Nyerere anaweza
kunishawishi mimi kwa kipi? Ngoja nikwambie kitu, kinachoendelea ni kiki
ya Steve Nyerere na watu wake maana kama umesikia ile ‘place’ na
waandishi aliyoitisha, anasema Makonda ni rafiki yake, sasa unaweza
kupima kinachoendelea hapo.”
MUSUKUMA AKATAA RADHI YA STEVE
Alipoulizwa kuhusu radhi aliyoiomba Steve Nyerere kwa wote aliowataja
yeye ameipokeaje, alisema: “Kama ameomba radhi basi amewaomba wananchi
wangu wa Geita waliyoniweka kwenye nafasi yangu kwa lengo la kuwatetea wananchi na si kufanya kazi kwa ushawishi wa mtu.”
TID KWENDA KORTINI? Taarifa zaidi zilisema kuwa, Mbongo Fleva, TID
anajipanga kumfikisha Steve kortini baada ya sauti yake kumtaja akisema
anamchukia sana yeye huku pia kukiwa na habari kwamba, baadhi ya
wanasheria jijini hapa wamepanga kujitokeza kwa waliotajwa ili kuangalia
uwezekano wa kumfungulia kesi mama Wema ambaye anatajwa na Steve
mwenyewe kuwa, ndiye aliyemrekodi.
Post a Comment