0


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema jumla ya watuhumiwa 30 wa mauaji ya vikongwe na wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, wamehukumiwa kunyongwa, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji hayo.

Dk Mwakyembe amesema pia kuwa serikali itaendelea kutoa adhabu kali kwa watu watakaobainika kuendelea kuhusika na mauaji ya watu hao ili kumaliza tatizo hilo, ambalo limeipaka matope Tanzania kwa kuonekana sio kisiwa tena cha amani. Waziri huyo alisema hayo mjini Shinyanga jana, alipofanya ziara yake ya kikazi.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni tatizo la mauaji ya wenye ualbino na vikongwe yamepungua nchini na kwamba watahakikisha wanayakomesha kwa kutoa adhabu kali kwa wauaji.

“Tatizo hili la mauaji ya vikongwe na albino linatutia sana doa nchi yetu kimataifa ambayo imekuwa ikisifika kwa amani na utulivu, hivyo natoa mwito kwa wananchi waachane na mauaji ya watu hawa wasio na hatia pamoja na mahakama zifanye kazi kwa kutoa hukumu za haraka kwa watu watakaohusika na mauaji hayo,” alisema Dk Mwakyembe.

Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema serikali itaanza mikakati ya kujenga mahakama za mwanzo kwa kila kata nchi nzima ili kuondoa misongamano za kesi mahakamani na kukarabati majengo ya mahakama ambayo yamechakaa.

Aliwataka wakuu wa wilaya, waunde kamati za maadili ya wilaya.

Akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, alitaja changamoto ambazo zinawakabili kuwa ni uchakavu wa majengo ya mahakama, uhaba wa mahakimu na magereza ya Shinyanga na Kahama kuwa finyu na hivyo kusababisha mlundikano wa wafungwa.

Post a Comment

 
Top