SERIKALI imeiamuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzishikilia akaunti za Kampuni kubwa ya mafuta ya Uingereza (BG Group) hadi pale itakapolipa Kodi ya Ongezeko la Mtaji (capital gain tax) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 502.
Taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la wiki, TRA tayari imetoa maelekezo kwa Benki ya Citi kushikilia akaunti za kampuni hiyo.
TRA inadai kiasi hicho kutokana na faida iliyotokana na BG Group kuziuza hisa zake asilimia 60 kwa kampuni nyingine za nishati za Royal Dutch Shell, Exxon Mobil, Ophir Energy na Statoil.
Biashara hiyo, pia ilihusisha maslahi ya BG, visima vya mafuta namba 1 na 4 vilivyopo kusini mwa Tanzania.
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Fedha na TRA, vilisema amri hiyo imetolewa kushikilia akaunti za BG Group hadi kodi hiyo itakapolipwa.
Baada ya akaunti kukaguliwa, ilibainika fedha zilizopo katika benki hiyo, ni Dola milioni 5 tu, ikiwa ni sawa na asilimia moja tu ya kiasi inachodai TRA.
Uamuzi huo unazua maswali katika rufaa, ambayo BG Group imeifungua katika Mahakama ya Kodi Tanzania ikipinga namna tathimini ilivyofanyika kupata kiasi hicho inachodaiwa.
BG Group, inasema haiwezi kulipa kodi kwa sababu iliwekeza Dola milioni 850 ya jumla ya faida iliyopata katika visima Tanzania.
BG Group iliendelea kudai kampuni yake dada, tayari imetumia dola bilioni 1.5 kama uwekezaji, na hivyo kuashiria upotevu wa mtaji.
Kwa mujibu wa Sheria ya Rufaa ya Kodi ya Mapato (2006), mtu yeyote asiyeridhishwa na kiasi cha kodi anachodaiwa anaweza kupinga kwa kumuandikia Kamishina Mkuu.
Ibara ya 12 (3) ya sheria hiyo inasema. “Wakati taarifa ya kupinga kiasi cha kodi kinachodaiwa inapowasilishwa, mtu anayepinga anatakiwa wakati akisubiri uamuzi wa mwisho wa Kamishina Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 13, alipe kiasi cha kodi ambacho hakikupingwa au theluthi moja ya kiasi kilichopingwa, bila kujali ukubwa wa kiwango”.
Lakini wanasheria na wataalamu wa nishati, wameitaka Serikali na BG Group kutatua mkwamo huo, ambao unaweza kuchelewesha uamuzi wa mwisho wa uwekezaji wa dola milioni 30 wa mradi wa usindikaji wa gesi ya asili ya matumizi mbalimbali (LNG), ambao kampuni hiyo ina mipango ya kuijenga kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Ujenzi huo wa mtambo wa LNG, utakaozalisha tani milioni 10 za gesi kwa mwaka, awali ulikuwa ukamilike mwaka 2020.
Lakini chini ya sheria za nchi, ujenzi hauwezi kupitishwa hadi kodi itakapolipwa kwanza.
Serikali imebakia kimya kuhusu suala hilo, lakini Kamishina Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata alisema suala hilo bado halijafika kwake, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akilitaka gazeti hilo kumuuliza Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk. James Mataragio, ambaye hakuwa tayari kusema lolote.
Kuna wasiwasi mizozo kuhusu kodi inaweza kuathiri uwekezaji wa kigeni unaotarajiwa kuwekezwa nchini.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kampuni ya Shell kupitia hisa BG, imejipanga kimkakati kujipatia vibali vya utafutaji wa mafuta Zanzibar kwa sasa kwa vile inamiliki pamoja na Serikali. Shell imekuwa ikihaha kwa miaka 10 sasa kujipatia vibali vya utafutaji mafuta visiwani humo.
Subiro Mwapinga, mshauri katika kampuni ya ushauri wa masuala ya gesi na mafuta ya Mnazi Bay Consulting Group, alisema mzozo wa sasa wa kodi umeuweka uwekezaji wa LNG katika hatari na unaweza kuathiri miradi mingine, ikiwamo ujenzi wa pipa la mafuta baina ya Uganda hadi Tanga wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 10.
“Iwapo ukokotoaji wa kodi wa TRA umefanywa kwa kufuata taratibu zote za kimataifa na kuendana na sheria, kuna nafasi ndogo kwa BG Group kuweza kukwepa kulipa kodi, lakini bado hilo lina athari zake linapokuja suala la kubadilisha miundo ya mradi wa LNG, ambayo imepangwa kujengwa kwa ubia na washirika mbalimbali.
Kwa mfano, linaweza kusababisha washirika wengine kujenga miradi yao wenyewe ya LNG,” anasema Mwapinga.
Vyanzo vya habari ndani ya Wizara ya Fedha na TRA vilisema serikali pia imeamua kwa muda kusimamisha maombi ya Shell na BG Group ya kufufua vibali vya kutafiti nishati katika visima viwili hadi mgogoro huo utakapomalizika.
Kibali cha kisima namba 1 kinaishia Desemba mwaka huu, huku cha kisima namba 4 kikiishia Oktoba 2017.
Vibali vya kutafuta mafuta hutolewa kwa kipindi cha miaka minne kisha kufufuliwa kwa miaka minne mingine na kisha kipindi kingine cha miaka mitatu, baada ya hapo kampuni inatarajia kuomba kibali cha uendelezaji.
Kisha kwa mujibu wa kumbukumbu za serikali, kampuni itaongezewa wastani wa chini wa miaka 11 na kuomba vibali vya maendeleo lakini haiko tayari bado kwa hilo.
“Hali hiyo inaonesha Shell inatakiwa kuomba kuongezwa muda kwa kibali cha kutafuta mafuta kwa ajili ya kisima namba 1 na 4, lakini ongezo la muda huwa chini ya mamlaka ya waziri kwa vile liko nje ya kipindi cha miaka 11. Ni hapo serikali ndiyo iliyoshikilia mpini,” vyanzo vya habari vilisema.
Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa (CCM) na mratibu wa zamani wa Taasisi ya Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Tanzania,alisema usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi unahusisha mabilioni ya dola za uwekezaji na miamala mbalimbali katika shughuli za hapa na pale.
“Wakati kunapotokea mabadiliko, migogoro inaweza kuibuka iwapo mfumo wa sheria wa nchi husika hauko wazi kuhusu taratibu za miamala,” alisema Bashungwa.
Mbunge huyo alisema, migogoro ni ishara ya udhaifu wa kisheria na maandalizi ya taratibu. “Naamini Serikali na BG zitapata suluhu kwa amani kwa fedha hizo za ongezeko la mtaji zinazobishaniwa.
“Vinginevyo wanachama wa Chama cha Mafuta na Gesi Tanzania na wawekezaji watarajiwa watalichukulia kama kengele ya hatari ya kitakachowatokea siku za usoni,” alisema mbunge huyo.
Post a Comment