Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha
mahakamani wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa.
Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa
taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia
kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo.
Mratibu wa THRDC, Onesmo
Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa
wazi jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa
makosa ya jinai.
“Hadi sasa watetezi wanne wamenyimwa dhamana wakati
wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si sawa,” alisema
Olengurumwa.
Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria,
Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni
mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa
Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros,
Joshua Makko.
Alieleza kuwa watetezi hao wamenyang’anywa vitendea kazi
vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo simu za mkononi na
kompyuta mpakato.
Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya Law Guards
Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria zinazosimamia
haki za binadamu nchini.
“Kumshikilia mtu muda mrefu bila dhamana
pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume
na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka
1998,” alisema Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa
haki ya kuwatumia mawakili.
Licha ya ombi hilo kwa Polisi, mwanachama wa mtandao huo,
Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili
kuhakikisha haki inatendekea.
Aliziomba asasi za kimataifa kukemea na
kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea huko
Loliondo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema
jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na halichagui wa
kumkamata kama amefanya kosa la jinai.
“Lazima ukamatwe labda uwe na
kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai
nitakamwa tu,” alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea
kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.
Post a Comment