0



Diwani wa Kata ya Kiborlon (Chadema) katika Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.
 Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata. 
Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya majambazi hao kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni. 
Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hao walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris. 
Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri. Akisimulia tukio hilo, diwani huyo alisema siku hiyo akiwa maeneo ya Kiborlon, alipigiwa simu kuwa mfanyabiashara huyo amevamiwa na majambazi ndipo alipoendesha gari lake hadi eneo la tukio. 
“Nilipofika pale wale majambazi watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka. Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika bunduki. Kuona hivyo akafyatua risasi hewani,” alisema Kagoma. 
“Yule mwenye bunduki akaingia uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola naye akawasha risasi nyingine hewani kunitisha,” alisema. 
Baada ya hali hiyo, diwani huyo alilazimika  kujificha kwenye gari na majambazi hao walidandia pikipiki na kuanza kukimbia kuelekea Barabara ya Msaranga, naye akawafuata kuelekea huko. 
“Wakati huo tayari vijana wangu wa bodaboda wakawa nao wamesikia hilo tukio tukaanza kusaidiana kuwafukuza lakini mbele kidogo pale Msaranga wale majambazi wakasimamisha pikipiki yao umbali wa mita 30 kutoka nilipokuwa na mmoja wao mwenye bunduki alifyatua risasi mbili na mwenye bastola risasi mbili kuelekea uelekeo wangu. 
“Nililazimika kujificha kwenye kiti, wale majambazi wakajua wameniua. Wakapanda tena pikipiki ili watoroke. Nikawasha tena gari huku vijana wangu nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema. 
Kagoma alisema majambazi hao walipita maeneo ambayo gari haliwezi kupita wakaelekea eneo la Mabogini Moshi Vijijini hadi lango la TPC na baadaye wakaelekea Rundugai wilayani Hai. 
“Kuna eneo vijana wangu wanasema kulikuwa na vumbi sana, ndipo walipowapoteza na majambazi wakatoroka kupitia njia ya reli ili kukwepa polisi waliokuwa wakiwasubiri mbele,” alisema na kuongeza: “Hatukuwa na silaha, lakini tulijitahidi kupambana nao kwa ujasiri. Tatizo nafikiri tulikosea kidogo. Ilitakiwa wakati tukifukuzana nao tuwape polisi uelekeo wa majambazi.” 
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa Jeshi lake litatoa taarifa rasmi kwa wanahabari leo kuhusiana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo. 
“Kuna mambo tumeyafanya tangu tukio hilo litokee lakini kesho (leo) saa sita mchana tutatoa taarifa rasmi pamoja na mafanikio tuliyofikia hadi sasa. Tunaendelea vizuri na upelelezi,” alisema.
Kamanda Mutafungwa, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ikiwamo kuwafichua wahalifu na mbinu wanazozitua akisema polisi wamejipanga kukabili wimbi jipya la ujambazi.

Post a Comment

 
Top