0

CAG
Wamtaka CAG afanye ukaguzi maalumu upotevu wa sh bilioni 9
Na Elizabeth Hombo, Dodoma

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeibua ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni tisa katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), unaohusisha fedha zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya miradi ya mazingira katika maeneo ya Dar es Salaam, Bagamoyo, Pangani, Rufiji na Zanzibar.

Kambi hiyo imeeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuomba tena kiasi hicho cha fedha katika bajeti ya mwaka 2016/17, kwa ajili ya kazi hiyo hiyo ambayo fedha zake zilishatolewa na nchi wahisani ambazo ni Marekani na Ujerumani.

Kwa mujibu wa kambi hiyo, miradi hiyo miwili ilikumbwa na ufisadi mkubwa ambao ulikuwa ukiendeshwa baina ya mtumishi mmoja aliyeko katika Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mabadiliko ya Tabianchi akishirikiana na kigogo mmoja aliyekuwa Ikulu wakati wa utawala wa awamu ya nne.
GekuliTaarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Kivuli katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Pauline Gekul wakati akiwasilisha taarifa ya kambi h
iyo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi katika ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17
.
“Mtumishi huyo wa Serikali alishirikiana na kigogo mmoja aliyekuwa Ikulu wakati wa utawala wa awamu ya nne katika kutafuna fedha ambazo zilikuwa zimetolewa  na wafadhili,” alisema Gekul.
Kutokana na kashfa hiyo aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais imtake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanyie ukaguzi maalumu (Special Audit) wa miradi hiyo miwili.

“Tunataka CAG akague miradi hii ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi , pamoja na miradi mingine yote iliyosimamiwa na Kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi kilichopo chini ya Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kwani kuna majipu ya kutumbua.

“Tunaomba Bunge lisitishe kupitisha maombi ya fedha ya mradi huu hadi ukaguzi maalumu utakapofanyika kuhusu fedha za mradi ambazo zilikuwa zimetolewa na wafadhili utakapokamilika,”alisema.

Kuhusu mradi wa Dar es Salaam pamoja na mambo mengine alisema ulitakiwa kusimamiwa na  Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikisha Jiji la Dar Es Salaam na halmashauri zake kwa ajili ya kutengeneza baadhi ya miundombinu ya majitaka ya jiji hilo.

Gekul ambaye pia ni Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), alisema kwa mujibu taarifa ya wizara hiyo inaonesha kuna matatizo makubwa ikiwamo uchache wa watumishi katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira ambayo imelifanya baraza kushindwa kutimiza majukumu yake.

“Vilevile ufinyu wa bajeti ambayo inatengwa na Bunge pia umesababisha baraza kukosa fedha na badala yake linategemea kujiendesha kwa kutegemea faini na tozo ndizo zinazotumika kuendesha baraza,”alisema.

Gekuli alisema kambi hiyo inaishauri Serikali kama kweli ina dhamira ya kutaka uchumi wa viwanda, ni lazima iongeze bajeti katika wizara hiyo na hasa kwa ajili ya shughuli za baraza hilo ili liweze kufanya tathimini ya mazingira kabla ujenzi na ufufuaji wa viwanda husika haujaanza kutekelezwa.

“Pamoja na hilo pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Serikali ina mipango gani endelevu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo kuandaa sera mahususi na kuwa na sheria ya kusimamia utekelezaji wa sera husika.

“Aidha tunataka kujua tumejipanga vipi kutekeleza kwa vitendo mikataba yote ya kimataifa ambayo tumeiridhia inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Gekul.

Post a Comment

 
Top