Jeshi la Nigeria limeanzisha operesheni kubwa dhidi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika msitu wa Sambisa.
. Duru za kijeshi zinasema kuwa, jeshi la Nigeria limeshaanza operesheni yake ya kijeshi katika msitu huo wa Sambisa. Wakati huo huo, jana Mansur Mohammed Dan Ali Waziri wa Ulinzi wa Nigeria alitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo linafanya juhudi ili liweze kuingia kikamilifu katika msitu huo unaohesabiwa kuwa kituo kikubwa kabisa cha kutoa mafunzo cha wanamgambo wa Boko Haram.
Waziri huyo amesema kuwa, muda sio mrefu watafanikiwa kung'oa mizizi ya Boko Haram katika msitu huo.
Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mbali na Nigeria wanamgambo hao sasa wanaendesha harakati zao za kigaidi katika nchi za Chad, Niger, Cameroon na hata Benin.
Post a Comment