0

 

  
            Azam na Yanga kucheza ugenini Nusu Fainali kombe la Shirikisho      
          
Droo ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imefanyika jana huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata nafasi ya kucheza nyumbani.
 
Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, imewashuhudia vigogo wa Ligi Kuu ya Tanzania bara, Azam FC na Young Africans wakipata nafasi ya kucheza michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.

Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku wagosi wa Kaya Coastal Union wakicheza dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga siku hiyo hiyo.

Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya kombe hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).
Na Ligi Kuu ya Tanzania bara inatarajiwa kuendelea tena leo Jumatano, kwa michezo miwili katika viwanja vya Manungu Turiani mkoani Morogoro na uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Young Africans wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, watakua wenyeji wa Mwadui FC inayokamata nafasi ya sita katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar walio katika nafsi ya nne ya msimamo wa ligi kuu watawakaribisha Azam FC walio juu yao nafasi ya tatu, mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Manungu Turiani mkoani Morogoro.

Post a Comment

 
Top