0
Frid
                                                            James Lembeli.
 
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya ubunge katika jimbo la kahama Mjini, baada ya kuondoa hoja zote zilizowasilishwa na mlalamikaji.

Akitoa hukumu hiyo mbele ya umati uliofurika mahakamani hapo jana, Jaji Moses Mzuna alisema kuwa mlalamikaji, James Lembeli, alishindwa kuwasilisha ushahidi wenye mashiko dhidi ya madai yake mahakamani hapo.

Alisema kuwa pamoja na madai ambayo awali mlalamikaji alidai kuwa ya msingi, mahakama kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, imebaini pasipo shaka yoyote kuwa ushahidi wake hauna mashiko na ni wa kuunga unga, hivyo mahakama inaendelea kumtambua Jumanne Kishimba kuwa ndiye mbunge halali wa Kahama Mjini.

“Mleta maombi ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi ameshindwa kuleta ushahidi dhidi ya mlalamikiwa wa Kwanza, Jumanne Kishimba,” alisema jaji Mzuna.

Katika hukumu hiyo, Jaji alionya jamii na vyama vya siasa kuheshimu demokrasia na kuzingatia haki na sheria zilizopo kwa kile alichosema  uchaguzi ni kitu kitakatifu na kina utukufu kwa vile hukubaliwa na watu wengi ambao ni wapigakura, hivyo sharti matokeo ya kura yaheshimiwe.

Aidha alikemea tabia ya vyma na viongozi kuhama vyama vyao vya siasa na baadaye kuhamia chama kingine na kwenda mahakamani, hivyo kuwa vigeugeu aliowafananisha na kugeuza koti.

Lembeli alifungua kesi kupinga ushindi wa Kishimba (CCM) akidai kuwa mgombea huyo alishinda kutokana na kutoa rushwa kwa wapigakura ili wamchague.

Pia katika kesi hiyo Lembeli kupitia kwa wakili wake Mpale Mpoki, alipinga vifungu vya sheria vilivyotumika kwenye kesi ya utoaji rushwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, mwaka jana.

Lembeli, baada ya hukumu hiyo, alidai kuwa atawasiliana na wakili wake kuwasilisha madai Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Jaji Mzuna.

Kishimba kwa upande wake, alisema sasa ni kazi tu na fedha za gharama za kuendesha kesi hiyo atazitumia kutengenezea madawati na kununulia vifaa tiba hosiptalini na kuahidi kuendelea na mpango wake wa kuhakikisha anaboresha miundombinu ya barabara jimboni humo.

Post a Comment

 
Top