Mabingwa hao wa Bara wanacheza mchezo wao wa kwanza wa viporo leo Uwanja wa Taifa, huku Azam wakiwa Mwanza.
Yanga na Simba.
Mbali na mechi hiyo, pia leo ligi hiyo itashuhudia wawakilishi
wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC
wakianza ratiba ngumu kwa kucheza dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kadhalika, JKT Ruvu watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya African
Sports ya Tanga kama ilivyo kwa Mwadui watakaowakaribisha Mtibwa Sugar,
huku Prisons ikisafiri kwenda kuwavaa Ndanda FC.
Yanga haikuwa dimbani kwa mchezo wowote wa Ligi Kuu tangu
walipocheza mechi ya marudiano dhidi ya APR ya Rwanda – Ligi ya Mabingwa
Afrika na kutoka sare ya bao 1-1.
Mabingwa hao wenye pointi 50 na michezo mitatu mkononi, wanaweza
kupunguza pengo la pointi dhidi ya mahasimu wao, Simba walio kileleni
kwa pointi 57.
Awali, kocha wa Yanga Hans van der Pluijm alisema kuwa kikosi chake
kinakabiliwa na ratiba ngumu ya ligi kuu, lakini lazima washinde mechi
zote zilizo mbele yao.
“Tumepangiwa ratiba ngumu ya mechi za viporo, ni kama tumekomolewa
kwa ratiba hii. Tunahujumiwa ili tushindwe kutetea ubingwa wetu,”
alilalamika Pluijm.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
limekubali kusogeza mbele mechi ya Jumatano dhidi ya Mtibwa, hivyo
itachezwa baada ya Yanga kumaliza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa
Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri mwishoni mwa wiki ijayo.
Kwa upande wa Azam FC, ratiba ya inabaki palepale pamoja na wao pia
kukabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance ya
Tunisia.
Msemaji wa Azam FC, Jaffer Idd alisema jana kuwa wamejipanga vizuri
pamoja na kuwa na ratiba ngumu inayowalazimu kucheza mechi nne ndani ya
siku 10.
Kama ilivyo kwa Yanga, Azam nao wako nyuma kwa michezo mitatu
wakiwa na pointi 50, hivyo ushindi utasaidia kupunguza pengo la pointi
dhidi ya Simba.
Post a Comment