Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Brussels umefunguliwa.
Uwanja huo ulikuwa umefungwa tangu shambulizi la bomu siku 12 zilizopita kusababisha vifo vya watu 16.Ndege zimeanza kuruka tena.
Mkurugenzi mkuu wa uwanja huo Arnaud Feist alisema ''Safari hii ya kwanza ya ndege tangu kushambuliwa na magaidi ni ishara tosha kwao kuwa uwanja huu wa ndege umefufuka na kuwa hatutashindwa na magaidi''.
Shirika la ndege la Brussels linakisia kuwa kufungwa kwa uwanja huo uliigharimu takriban Euro milioni €5m sawa na dola milioni $5.7m pesa za Marekani kila siku.
Kama ilivyotarajiwa kulikuwa na mabadiliko makubwa kwa wateja na abiria waliokuwa wakitumia angatua hiyo ya kimataifa.
Abiria walihitajika kufika uwanjani takriban saa tatu kabla ya muda wao wa kusafiri.
Usafiri wa gari moshi na mabasi ya umma bado haupo kwa hivyo kila aliyesafiri leo aliwasili kwa gari au teksi.
Aidha wahudumu wa uwanja huo wa ndege walikongamana katika eneo la Zaventem kushuhudia ndege za kwanza zilizokuwa zimeratibiwa kuanza safari zao hapo.
Ndege ya kwanza ilipaa mwendo wa saa tano na dakika arobaini saa za huko ikielekea Faro nchini Ureno.
Kabla ya ndege ya kwanza ya shirika la ndege la Ubelgiji kuruka, Mkurugenzi wa shirika hilo alisikika kwenye kipaza sauti akisema, ''kwa pamoja Tunasimama imara, Tumerejea''.
Ni ndege tatu tu ndizo zilizoratibiwa kurukaleo , kwenda Italia, Ureno na Ugiriki.
Kikawaida uwanja huo hutumika na ndege 600 kila siku.
Maafisa wanaoendesha uwanja huo wa ndege wamesema huduma hazitorejea katika hali yake ya kawaida mkapa mwishoni mwa mwezi wa sita.
Hapo kesho kutakuwepo na safari mbili tofauti moja ikielekea Turin Kaskazini mwa Utalia na nyengine ikielekea mji mkuu wa Ugiriki Athens.
Post a Comment