Wagombea tisa wanaopigania wadhifa wa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu
kabisa duniani wamelazimika kujibu masuala kadiri 800 na kwa muda wa
siku tatu kutoka kwa mabalozi na wawakilishi wa makundi tofauti ya
kiraia-
KIkao cha Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa
Mwenyekiti wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa Mogens Lykketoft,
aliyesimamia kikao hicho cha masuala na majibu amesema amevutiwa kuona
jinsi mataifa takriban yote 193 wanachama wa Umoja wa mataifa
wameshiriki katika mjadala huo,huku watu 227.000 kutoka nchi 29
wakifuatilizia zoezi hilo kupitia mtandao."Tayari kuna tofauti kubwa iliyojitokeza" Mogens Lykketoft amewaambia maripota jana usiku mjini New-York."Tumefungua ukurasa mpya wa uwazi na nchi kuhusishwa moja kwa moja katika utaratibu wa kumchagua katibu mkuu wa Umoja wa mataifa:" amesisitiza.
Kwa mujibu wa muongozo wa Umoja wa Mataifa,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa huchaguliwa na wanachama 193 wanaokutana katika hadhara kuu ya Umoja huo,kutokana na pendekezo la wanachama 15 wa baraza la usalama.Kimsingi hali hiyo inamaanisha kwamba wanachama watano
wa kudumu wa baraza la Usalama,Marekani,Urusi,China,Uengereza na Ufaransa wana haki ya kutumia kura ya turufu kuzuwia kuchaguliwa mgombea wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Hali hiyo haitobadilika katika kuchaguliwa kiongozi atakaemrithi katibu mkuu Ban
Ki-Moon ambae mhula wake wa pili wa miaka mitano unamalizika decemba 31 mwaka huu.
Zoezi la Masuala na majibu litasaidia kumpata mstahiki
Lykketoft amesema vikao vya masuala na majibu vinaweza kugeuka kuwa zoezi mbadala ikiwa nchi nyingi zitamuunga mkono mgombea mmoja-hali inayoweza kulishinikiza baraza la usalama lisimteuwe mgombea mwengine.
Bado lakini ni mapema kusema kama hali hiyo itawezekana hasa kwakua wagombea zaidi wanatarajiwa kujitokeza. Lykketoff anawahimiza wote wanaopendelea kugombea wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa wajitokeze haraka.
Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa mataifa Matthew Rycroft amesema zoezi la masuala na majibu kutoka kwa wagombea litazidisha ubora wa maamuzi ya baraza la usalama.
Wanachama wengine wa baraza la Usalama walikuwa waangalifu walipozungumzia umuhimu wa vikao hivyo vya masuala na majibu.Balozi wa Angola katika Umoja wa Mataifa Ismael Gaspar
Martins anasema vikao hivyo vinaweza kulipatia baraza la usalama picha ya kwanza muhimu ya mgombea anaestahiki kuchaguliwa.Balozi wa Urusi ,Vitaly Churkin anasema baadhi ya wanachama wanaonyesha kushawishiwa na zoezi hilo,lakini yeye binafsi halikumshawishi sana."Nnahisi linaweza kusaidia.Tusubiri tuone-amesema na kuongeza "amevutiwa na wagombea wote waliojitokeza.
Makundi ya wanaharakati wanapigania mwanamke achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa
Kijadi,wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukishikiliwav kwa zamu miongoni mwa mabara ya Asia,Afrika,Latin Amertica na Ulaya. Mataifa ya Ulaya ya Mashariki,ikiwa ni pamoja na Urusi yanadai katibu mkuu hajawahi kutokea katika eneo lao. Na kuna wanaodai pia jumuia hiyo ya kimataifa haijawahi kuongozwa na Mwanamke,ndio maana makundi kutoka mataifa 56 yanafanya kampeni safari hii katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa awe mwanamke.
Post a Comment