0


1MATATIZO makubwa yanayochangia kudorora kwa uchumi nchini ni ukosefu wa uwajibikaji serikalini na katika mashirika ya umma.#

Miradi mingi imekwama kwa kukosa usimamizi wa karibu kwa upande wa watendaji waliopoewa dhamana ya kusimamia ,ingawa wanapewa nyenzo ambazo hazina hesabu.

Tatizo la ukosefu wa uwajibikaji ni kubwa hapa nchini kiasi kwamba zaidi ya asilimia 75 ya watendaji katika Serikali na sekta za umma si tu hawawajibiki ipasavyo, bali pia dhamira zao haziwasuti kutokana na kukosa uzalendo na uadilifu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lilikutana na wadau wa wauzaji vilainishi mitambo na injini ambapo washiriki wengi walisema wapo wauzaji wa mafuta feki lakini wanalelewa na wahusika serikalini.

“Inakuwaje vyombo husika vipo na wizara zipo zinazosimamia masuala hayo lakini vinawaangalia wahusika, wanaingiza mafuta feki baadae wanatuunganisha na sisi kwamba tunafanya wote? anahoji Juma Ali kutoka kampuni moja ya uuzaji wa mafuta Arusha.

Wafanyabishara waliokuwapo katika mkutano huo  wanasema hupata bidhaa hiyo kutoka katika Visiwa vya Zanzibar na nchi jirani.
Vilainishi
 “Ni kweli tumesikia tangazo la TBS lakini tunachokiona hapa ni mawasiliano ya kiutendaji kati ya TBS na ZBS, ukienda Zanzibar bidhaa hii ni ruksa nasi tunapata huko na kuingiza nchini,” anasema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Taarifa kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali si za kupuuza hata kidogo, hasa inaposema kwamba sampuli 102 za vilainishi kutoka katika kampuni tatu zilizofanyiwa uchunguzi kwa kipindi cha Septemba 2013 hadi Januari 2014 zilionyesha kwamba vilainishi feki vilivyoingizwa nchini ni kati ya aslimia 78 hadi 79.

Taarifa hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko, ambaye anasema hali ni mbaya sana mitaani.

“Juhudi zinahitajika kukomesha biashara hii haramu kwani vilainishi feki ni hatari kwa uchumi wa nchi yetu inayotegemea pia mitambo na injini za vyombo vya moto kuendesha miradi na shughuliza maendeleo.

“Sisi tunadhani kampuni zinazoingiza vilainishi hivyo nchini lazima zichukuliwe hatua kali, zinatenda kosa la jinai hivyo haitoshi tu kuziagiza kuondoa malighafi ya vilainishi hivyo katika soko bila kuziwajibisha kisheria,” anasema Masikitiko.

Naye Meneja Ufundi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Gerald Maganga, anasema Watanania wanaoitakia mema nchi yao lazima wajiulize kama kweli wafanyabisbara wanaoingiza vilainishi feki au wanaotengeneza bidhaa hizo nchini wanaitakia mema nchi yetu.
Leo Lyayaka Ofisa kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, anasema sheria iko wazi kwamba kampuni zinazoingiza malighafi za vilainishi nchini lazima ziwe na lebo na kadi ya usalama wa kemikali zinazotumika kutengeneza vilainishi hivyo, tofauti na hapo ni feki.

Maofisa kutoka EWURA, TBS, Mkemia Mkuu wa serikali na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa pamoja wamekubaliana kuingia mitaani kuanza msako wa vilainisho hivyo.

Itakumbukwa mwaka juzi shirika la viwango Tanzania lilitoa orodha ya vilainishi vilivyopigwa marufuku ambavyo ni  Motor Oil (Super Plus Sae 40), Diesel Engine oil (Top Gatex super Plus SAE 40), Motor oil Gatex Super plus SAE 40) na Diesel oil (Laurence Lubricants).

Vingine ni Petro engine oil (Lubex SAE 40), Diesel Engine (Lubex SAE 40), Motor  Oil (Caltex Super Sae 40), Diesel Engine (Mohona Lubricants SAE 40), Motor oil (Duma Tech Sae 40),   Diesel  engine oil (Universal Lubricant HD 40), Diesel engine oil,  Auto Star Sae 40, Diesel engine oil na Super plus Sae.

“Ujumbe wangu kwa watumiaji wa vilainishi hivyo nawaarifu kuwa bidhaa hiyo si salama kwa injini za magari na mitambo yao kwani havikidhi mahitaji katika kupoza na kulainisha,” anasema Masikitiko.

Amesema pamoja na kupiga marufuku vilainishi hivyo bado wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiviuza kwa watumiaji katika maduka na vituo vya mafuta mbalimbali nchini.
“Kwa kawaida kwa gari ndogo unatakiwa kuweka kilainishi kiasi cha lita tano, hizi unatakiwa kutembela kilomita 3,000  lakini unakuta ukiweka kilainishi kisicho na ubora utatembea kilomita 500.
“Sasa ili kufikisha kilomita 3,000 unatakiwa kununua mara sita, hapo unatumia fedha pasipostahili,” anasema Masikitiko.

Post a Comment

 
Top