0


Rais Hassan Rouhani: Nguvu za Iran haziko dhidi ya majirani na nchi za Kiislamu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nguvu na uwezo wa Iran hauko dhidi ya majirani na nchi za ulimwengu wa Kiislamu. 
 
Rais Rouhani ameyasema hayo asubuhi ya leo katika maadhimisho ya Siku ya Jeshi na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa amri na wasia wa Imam Khomeini (ra) na kwa tadbiri na uongozi wa amiri jeshi mkuu wa majeshi yote, jeshi la Iran ni jeshi la Uislamu, ni jeshi la mfumo wa Kiislamu na jeshi la wananchi wote wa Iran.

Amesema hii leo taifa la Iran lina jeshi lenye nguvu, uwezo, misukumo ya kidini, Kiislamu na ni jeshi ambalo linafikiria maslahi ya kitaifa ya nchi.

Rais wa Iran amesema kuwa, kama leo watu wanaona madola makubwa ya kibeberu na vibaraka wake katika Mashariki ya Kati hawawezi kuitazama Iran kwa jicho la tamaa na usaliti ni kutokana na kuweko jeshi lenye nguvu na uwezo.

Rais Hassan Rouhani amesema pia katika maadhimisho hayo ya Siku ya Jeshi hapa nchini kwamba, jeshi la nchi hii litakata mikono ya wavamizi endapo watainyoosha kwa ajili ya maslahi ya taifa hili.
Ikumbukwe kuwa, Jumapili ya leo tarehe 17 Aprili inasadifiana na maadhimisho ya Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu. Katika maadhimisho ya leo kumefanyika magwaride na maonyesho mbalimbali ya silaha ambayo yamehudhuriwa na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi hapa nchini.

Post a Comment

 
Top