0

Serikali ya Burundi yaomba iondolewe vikwazo ilivyowekewa na Jumuiya ya Francophone
Serikali ya Burundi imeomba iondolewe vikwazo ilivyowekewa na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone). 
 
Ombi hilo la serikali ya Burundi limetolewa na Edouard Nduwimana Naibu Spika wa Bunge la nchi hiyo mara baada ya kurejea kutoka New York Marekani.

Naibu Spika wa Bunge la Burundi amesema kuwa, hatua ya Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone) ya kuiwekea vikwazo nchi hiyo inapingana na azimio nambari 2249 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Naibu Spika Nduwimana amedai kuwa, kwa kuzingatia matukio yaliyotokea katika anga inayotawala katika jamii ya Burundi kuna matumaini kwamba, katika kikao kijacho cha Julai mwaka huu Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone) itaondoa vikwazo vyake ilivyoiwekea Burundi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone) imetangaza kuwa, hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa na serikali ya Burundi licha ya ahadi yake ya kuandaa anga ya mazungumzo na mrengo wa upinzani.

Mwaka mmoja umetimia tangu Burundi itumbukie katika hali ya mchafukoge mwezi Aprili mwaka jana, kufuatia hatua ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena urais katika uchaguzi uliopita nchini humo, hatua ambayo ililalamikiwa vikali na wapinzani wanaosema ilikiuka katiba na makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania.

Post a Comment

 
Top