0
Seif_Sharif_Hamad

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameiomba Jumuiya ya Kimataifa na washirika wa maendeleo kuchukua hatua kali dhidi ya watawala, ikiwamo kuwawekea vikwazo vya kusafiri na  kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya nchi.

Maalim Seif alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa CUF baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.

“Naipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa na washirika wa maendeleo kwa msimamo waliouchukua wa kukataa kubariki ubakaji  wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika uapishwaji wa mtu asiye na ridhaa ya wapiga kura wa Zanzibar.

“Napongeza hatua ambazo wameanza kuzichukua dhidi ya Serikali ya CCM ambazo zilisimamia ubakaji wa demokrasia na haki za watu.

“Natoa wito kwao kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu, zikiwemo kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akaunti zao za nje ya nchi na hatua za kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu,”alisema.

Alisema suala la kuwa na akaunti nje ya nchi, liko wazi na kwamba chama hicho kinazo taarifa hadi  kiwango cha fedha kilichochukuliwa.

Alisema kabla ya uchaguzi mkuu, kuna fedha zilihamishiwa nchini Dubai na nchi nyingine ambapo walioweka fedha hizo wamejenga majumba.

Alisema Baraza Kuu la chama hicho, lilipitisha maazimio 13 na baada ya maazimio hayo kinachofuatia ni utekelezaji wake.

Alisema  hivi sasa wanapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji kwa kutumia njia za amani, demokrasia na kikatiba ili kuwafikisha CUF kwenye malengo yao ya kuona uamuzi wa watu wa Zanzibar unaheshimiwa.

“Nina hakika mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambao kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka.

“Maazimio hayatambui matokeo ya uchaguzi , hayamtambui Rais za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kuwa rais , hayawatambui waliotangazwa kuwa wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa madiwani.

“Narudia kusisitiza msimamo wetu, hatukubaliani na uamuzi wa kupoteza demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala waovu.

“Kwa misingi hiyo, Wazanzibari wataendelea kuipinga Serikali isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia za amani, kidemokrasia na zinazoendana na misingi ya Katiba na sheria za nchi yetu.

“ Jana (Jumamosi), wametangaza kile kilichoitwa Baraza la Mawaziri, msimamo wetu uko palepale kama tusivyomtambua aliyetangaza baraza hilo vivyo hivyo hatulitambui baraza lake,”alisema.

Maalim Seif aliwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani ya nchi na umoja wao, na kwamba akiwa kama kiongozi anayependa na aliyejitolea kuwatumikia katika umri wake wote hawezi kuwaongoza kuelekea kwenye fujo na ghasia au vitendo vitakavyosababisha kuiharibu nchi na kuathiri watu.

Kuhusu madai kuwa amenunuliwa, Maalim Seif alisema hakuna mwana CCM hata mmoja aliyewahi kumfuata kusema watampa hiki ama kile.

“Mimi sinunuliki, hawana bei ya kuninunua, nalinda heshima yangu na kuijali kuliko fedha, nataka nife na heshima yangu, hakuna bei ya kuninunua mimi,”alisema.

Alisema waliamua kususia uchaguzi uliofanyika Machi 20, mwaka huu kwa sababu ni batili na pia waliamua kuheshimu misingi ya Katiba ambayo watu wa Zanzibar wameamua ndio iongoze na kuendesha nchi.

“Tulijua uamuzi huo utakuwa na athari kwa Wazanzibari, CUF tuliamini athari hii haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na sheria za nchi, gharama ya kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.

“Tulipima na kutafakari tukaona ni heri kumeza machungu ya athari binafsi kwetu, lakini tusimame kidete na kifua mbele kutetea uamuzi wa  Wazanzibari walioufanya Oktoba 25 mwaka jana,”alisema.
Alisema siku zote CCM wanapenda namba, lakini hawajui hesabu, kwani walijifedhehesha wenyewe kutangaza matokeo bila kuzingatia uhalisia.

“Siku zote takwimu zina sifa moja huwa hazisemi uongo. Matokeo ya Machi 20 yaliyotangazwa eti jumla ya waliopiga kura ni 341,865, Dk. Shein kapata kura 299,982  ambayo ni sawa na asilimia 91.4.
“Takwimu za uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana waliopiga kura ni 402,354 na Dk. Shein alipata kura 182,011 sawa na asilimia 46.28, wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapiga kura kwa upande Zanzibar, walikuwa 417,882 ambapo mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.

“Watawala wa CCM walichotaka kutuaminisha ni tofauti ya waliokuwa hawakujitokeza kupiga kura kwamba ni 60,489.
“Kama takwimu zao zingekuwa sahihi ina maana wapiga kura waliomuunga mkono mgombea wa CUF ambao hawakwenda kupiga kura ni 60,489 ambao ni sawa na asilimia 15 tu.
“Hivi utamdanganya nani kwamba Maalim Seif anaungwa mkono na asilimia 15 tu ya wapiga kura wa Zanzibar?,”alihoji.

Post a Comment

 
Top