HATIMAE yametimia. Hii ni baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwapandisha kizimbani wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 30.
Kufikishwa kwa wabunge hao mahakamani, kulivuta hisia za wananchi ambao walifurika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kushuhudia tukio hilo.
Wabunge hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Maghela Ndimbo.
Ndimbo aliwataja wabunge hao kuwa ni Mbunge wa Mvomero, Ahmed Saddiq Murad (53), Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54) na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Walipofikishwa mahakamani, washitakiwa hao walionekana kuwa ni wenye furaha, ambapo muda mwingi walikuwa wakicheka sana wakiwa katika benchi la mahakama wakisubiri hakimu aingie wasomewe mashtaka yanayowakabili.
Ndimbo alidai kwamba, washtakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 15, mwaka huu kati ya saa 20:00 na 22:00 usiku katika Hoteli ya GoldenTulip, iliyopo Masaki Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alidai washtakiwa wakiwa kama wajumbe wa Kamati ya Bunge ya LAAC waliomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Mbwana Magotta.
Wabunge hao waliomba rushwa hiyo ili watoe upendeleo chanya kuhusiana na taarifa ya fedha ya wilaya hiyo ya mwaka wa fedha 2015/16.
Baada ya kusomewa, washtakiwa walikana shitaka, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo waliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Simba, alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuwapa washtakiwa masharti ya dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano.
Washtakiwa walitimiza masharti ya dhamana wakaachiwa huru, kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 14 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Post a Comment