Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewataka wakuu wa nchi za Kiislamu
wanaokutana mjini Istanbul katika mkutano wa kilele kukomesha
migawanyiko ya kiitikadi katika na kupambana dhidi ya ugaidi kwa pamoja.
Akihutubia mkutano wa kilele wa 13 wa shirika la ushirikiano wa mataifa
ya Kiislamu OIC mjini Istabul, Rais Erdogan alizungumzia matukio ya
kigaidi ambayo alisema wanapaswa kuyatafutia ufumbuzi wenyewe kupitia
muungano wa Kiislamu. Alisema pia ni aibu kuwa wengi wa wahamiaji na
wakimbizi wanaojaribu kuwasili barani Ulaya ni Waislamu.''Ukweli kwamba wale wote wanaojaribu kufika Ulaya kupitia bahari za Mediterrania na Aegean kwa kutumia boti na meli zilizochakaa ni Waislamu, ni jambo la aibu kwetu. Ikiwa hawa, ambao idadi yao inaelezwa kuwa mamilioni wameachwa bila chaguo lingine isipokuwa kufanza safari kama hizo kwa gharama ya maisha yao, tunahitaji kukaa pamoja na kulitafakari jambo hilo,'' alisema Erdogan.
Uturuki inataka kuonyesha ushawishi wake miongoni mwa Waislamu takribani bilioni 1.7 duniani, hasa katika ardhi zilizowahi kuwa sehemu ya himaya ya Ottoman, wakati wa mkutano huo wa siku mbili wa shirika la OIC ambalo itakuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Baadhi ya viongozi wakuu wa mataifa ya Kiislamu wanaohudhuria mkutano wa kilele wa OIC mjini Istanbul.
Migawanyiko ya kiitikadiLakini mkutano huo unaowaleta pamoja viongozi zaidi ya 30 uligubikwa na migogoro inayochochewa na tafauti za kiitikadi nchini Syria na Yemen, inayoyapambanisha mataifa ya Kishia ikiongozwa na Iran, dhidi ya dola la Kisunni kama vile Saudi Arabia.
Erdogan aliwakaripia wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu walioteka maeneo makubwa ya Syria, na wapiganaji wa itikadi kali wa Boko Haram nchini Nigeria, kama makundi mawili ya kigaidi yanayotumikia malengo sawa ya kishetani.
Alisema OIC imekubali pendekezo la Uturuki la kuundwa kwa kituo cha kimataifa cha ushirikiano na uratibu wa Kipolisi cha mataifa ya Kiislamu kupambana na makundi ya wapiganaji, kikiwa na makao yake mjini Istanbul.
Ulinzi umeimarishwa kuzunguka eneo la mkutano huo mjini Istanbul, mji mkuu wa zamani wa himaya ya Ottoman ambao ulikuwa makao ya Masultan waliotawala Waislamu kwa karne kadhaa kuanzia Balkan hadi Arabuni.
Kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu
Awali Erdogan alilaani chuki dhidi ya Waislamu inazidi kushamiri katika mataifa ya Magharibi, lakini pia alikiri kuwa jamii ya Kiislamu imekumbwa na ubaguzi wa kiitikadi, ambao unasabisha msuguano mkubwa.
Katika makala ya maoni katika kituo cha televisheni cha Marekani CNN kuelekea mkutano huo, Erdogan alikiri kuwa vijana wengi wa Kiislamu wako hatarini kwa ujumbe wa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu na Al-Qaeda, na kusema hili ni suala ambalo mataifa ya Kiislamu hayawezi na wala hayapaswi kuliacha liendelee.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kutilia mkazo zaidi kwenye masuala ya kikanda na matukio ya karibuni katika maeneo ya Wapalestina, Syria, Yemen, Libya na jimbo la Nagorno-Karabach miongoni mwa mengine.
Post a Comment