Kiongozi wa
mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu na makosa ya jinai ICC
yenye makao yake makuu nchini Uholanzi, bi Fatou Bensouda ameilaumu
serikali ya Kenya kwa kuhujumu kesi dhidi ya watuhumiwa wakuu wa ghasia
za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 naibu rais William Ruto na
mwandishi Joshua arap Sang.
''Tunasikita kuwa kutokana na shinikizo na hujuma dhidi ya mashahidi wetu kutoka kwa watu wenye uwezo mkubwa nchini Kenya, jopo la majaji wa mahakama ya kimataifa ya ICC lilishindwa kutoa hukumu kutokana na ushahidi halisi tulioyokuwa nayo.
Katika tukio hili, mashahidi 17 wa upande wa mashtaka waliokuwa wameahidi kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa walijiondoa wakihofia maisha yao.
Yamkini walikuwa wanatishiwa maisha yao, wengine walitengwa na jamii
Licha ya serikali ya Kenya kuahidi kuwa ingeshirikiana na mahakama ya kimataifa ya ICC ukweli ni kwamba serikali ya Kenya haikutoa 100% ya ushirikiano na mahakama ya ICC.
Hii ilisababisha afisi ya kiongozi wa mashtaka kukosa ushahidi uliohitajika kuthibitisha tuhuma dhidi ya washukiwa wakuu.
Vizuizi tulivyowekewa na washirika wa watuhumiwa wakuu wa mauaji na makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotokea punde baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 ulisababisha tukashindwa kuwawajibisha wale waliosababisha ghasia hizo na hivyo tumeshindwa kuwapa haki wale wahanga wa ghasia hiz o.'' Taarifa hiyo ya kiongozi wa mashtaka ilisema.
Bi Fatou Bensouda hata hivyo hakufa moyo anaiitaka serikali ya Kenya ichukue hatua kwa niaba ya wahanga wa machafuko hayo ya mwaka wa 2007 na kuwakamata mwandishi wa habari Walter Barasa, wakili Paul Gicheru na Philip Bett na kuwakabidhi kwa maafisa wa mahakama hiyo ya Uholanzi.
Watatu hao wanatafutwa na mahakama hiyo ya ICC kwa madai ya kutoa hongo kwa mashahidi na kwa kuwatishia mashahidi wa ICC hadi wakajiondoa.
Tayari vibali vya kukamatwa kwao vimeshatolewa.
Hapo jana jopo la majaji Olga Herrera Carbuccia, Chile Eboe-Osuji na Robert Fremr lilikubaliana na bi Bensouda kuwa mashahidi wengi walihongwa na kutishiwa maisha hadi wakajiondoa kufuatia shinikizo kubwa la kisiasa na hivyo wakawaondolea mashtaka naibu wa rais William Ruto na mwandishi habari Joshua arap Sang .
Post a Comment