0

Askari wa Umoja wa Mataifa auawa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Askari wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa ameuawa katika hujuma ya waasi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. 
 
Habari zinasema kuwa, askari huyo raia wa Morocco aliuawa baada ya waasi wa Lord's Resistance Army LRA wa Uganda kushambulia kijiji cha Mbomua, kusini mashariki mwa nchi karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani hujuma dhidi ya askari wa kusimamia amani na kusisitiza kuwa mauji hayo 'hayakubaliki.'

Msemaji wa UN amesema, askari huyo wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA aliuawa Jumapili kwa kufyatuliwa risasi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR, visa vya mauaji na uvamizi vinavyotekelezwa na LRA vimeongezeka mno katika Jamhuri ya Afrika ya kati katika miezi ya hivi karibuni.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, kundi la LRA limeteka nyara watu zaidi ya 200 mwaka huu pekee, huku asilimia 25 ya idadi hiyo ikiwa ni watoto wadogo.

Baada ya kutimuliwa kaskazini mwa Uganda waasi wa LRA walikimbilia misitu ya Afrika ya Kati. Waasi hao wa Kikristo wanaendesha mapambano ya kuiangusha serikali ya Uganda na kuanzisha utawala kwa mujibu wa amri 10 za Bibilia. Waasi wa LRA wametekeleza vitendo vya kikatili katika hali ambayo, kiongozi wao Joseph Kony anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binaadamu.

Post a Comment

 
Top