UONGOZI wa klabu ya Stand United umepanga kumuweka ‘kikaangoni’ mchezaji wao, Elius Maguli, kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo amekuwa akivionyesha kwa viongozi wa klabu hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana Ofisa Habari wa klabu hiyo, Deo Kaji, alisema Maguli kwa sasa amekuwa akionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu bila kuwa na wasiwasi wowote.
Alisema hivi karibuni wakiwa safarini kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Maguli alidiriki kuwatolea maneno machafu viongozi wa timu mara baada ya kuamuru gari liondoke kutokana na kusimama kwa muda mrefu wakiwasubiri wachezaji wenzao waliokuwa hawajui walipoenda.
“Tukiwa njiani gari lilisimama kwa ajili ya chakula na wachezaji walipewa dakika 15, lakini baadhi yao tuliwasubiri zaidi ya dakika 30 ndipo viongozi waliamuru gari liondoke na hapo Maguli alianza kutoa maneno machafu,” alisema.
Alisema hadi sasa mchezaji huyo hajajiunga kikosini licha ya wachezaji wote waliokuwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuruhusiwa kurejea katika klabu zao ambapo wamejitahidi kumtafuta kwenye simu yake ya kiganjani hapatikani.
“Tumekuwa tukitupiwa lawama kuwa Maguli hapangwi kwenye kikosi mara kwa mara, lakini hata akipangwa haonyeshi uwezo wake kama zamani hivyo Kocha Patrick Liewig analazimika kumpa nafasi mchezaji mwingine ambaye anaweza kuitendea haki nafasi yake,” alisema.
Kaji aliongeza kuwa suala hilo walilifikisha kwa kocha wa timu ya Taifa, Boniface Mkwasa, ili kufahamu tabia ya mchezaji wake na kusema kuwa atazungumza naye kwani mchezaji bila kuwa na klabu hawezi kuchezea timu ya Taifa.
Alisema kutokana na vitendo hivyo, uongozi unamsubiri atakapoamua kurejea katika klabu ili wamuweke kitimoto na kumchukulia hatua za kinidhamu.
Post a Comment