KILA kona hivi sasa katika nchi yetu, mjadala mkubwa ni vita dhidi ya
madawa ya kulevya. Ni vita aliyoianzisha Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul
Makonda lakini sasa imesambaa nchi nzima na duniani pia, ni kama moto wa
kiangazi kwenye pori lenye majani makavu.
Nani amesababisha madawa haya kusambaa dunia nzima? Nionavyo mimi leo
niwaletee mtu aliyechangia sana dunia kutikisika kutokana na madawa ya
kulevya, msome mtu huyo hapa.
Katika milima inayotazamana na mji wa Medellín nchini Colombia, yapo
majengo ya kifahari ndani ya milima hiyo ambayo sasa yanatumika kama
nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki lakini kabla ya watawa hawa kupewa
mwaka 2007, majengo haya yalikuwa ni gereza ambalo lilijengwa mwaka 1991
kumuhifadhi mfungwa maalumu raia wa Colombia.
Gereza hili licha ya kuwa mali ya serikali lakini michoro yake ilichorwa
na kubuniwa na mfungwa mwenyewe na hata askari magereza ambao walikuwa
wanalinda gereza hili walichaguliwa na mfungwa mwenyewe na hata polisi
wa nchi ya Colombia walikuwa hawaruhusiwi kusogelea gereza hilo hata
umbali wa maili 12.
Kwenye gereza hilo pia kulikuwa na chumba maalumu cha michezo ya watoto
maalumu kwa ajili ya watoto wa mfungwa huyo pindi akitembelewa na
familia yake. Na pia ndani ya gereza kuliwekwa darubini (Telescope) ya
kumuwezesha mfungwa huyo kuangalia katika mji wa Medellín ambako familia
yake iliishi na kila siku jioni alitoka nje kibarazani kuongea naye
kwenye simu huku akiwatazama kwa darubini hiyo.
Gereza hili lilijulikana kama La Catedral (The Cathedral) na
lilimuhifadhi mfungwa huyo ninayemzungumzia aliyesababisha biashara ya
mihadarati iwe jinsi ilivyo hivi leo duniani, mtu huyo ni Pablo Emilio
Escober Gaviria au kwa kifupi Pablo Escobar kama ulimwengu
ulivyomtambua.
Akiwa bado kwenye umri mdogo, Pablo mara kwa mara aliwaambia ndugu na
marafiki zake kuwa anataka awe na utajiri wa kiasi cha pesa milioni moja
za Colombia atakapofikisha umri wa miaka 22.
Ndoto hizi zilimfanya ashindwe kumaliza chuo kikuu alipokuwa anasoma
Universidad Autónoma Latino Americana of Madellín na kujiingiza katika
biashara za halali na haramu na hatimaye aliacha masomo chuoni. Moja ya
biashara zake haramu za kwanza kabisa akiwa kijana chini ya miaka 21
ilikuwa ni kutengeneza vyeti bandia vya stashahada vya chuo alichokuwa
anasoma na kuwauzia watu waliohitaji kwa ajili ya kwenda kupata ajira.
Pamoja na biashara hiyo pia Pablo alijihusisha na kusambaza mizigo ya
sigara zilizokuwa haziruhusiwi nchini Colombia (Marlboro), akawa
mhalifu. Kutokana na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu, Pablo
aligundua kuwa zao la coca linalimwa nchini Bolivia ambalo linatumika
kutengeneza Cocaine ni bora zaidi kuliko Coca inayolimwa nchini kwake
Colombia.
Hivyo basi, Pablo akadhamiria kuwa kama anaingia kwenye biashara hii ya
kusafirisha Cocaine ni lazima mihadarati yake iwe tofauti na bora zaidi
kuliko Cocaine nyingine watu waliyozoea kutumia.
Akadhamiria kufanya Cocaine yake iwe daraja la kwanza ili kuvutia
watumiaji na kufanya soko likue kwa haraka. Mwaka 1975 Pablo alisafiri
mpaka nchini Bolivia kukutana na Roberto Suaréz Goméz ambaye marafiki
zake walipenda kumuita El Padrino (The Godfather), kiongozi wa genge
lililoitwa La Corparacíon (The Corporation).
Pablo alimpata na kumpa wazo Suaréz kuwa atumie ushawishi wake alionao
serikalini akutane na kiongozi wa Cuba, Fidel Castro ili wamuombe
aruhusu ndege zao za mizigo zitue kwenye viwanja vya ndege vya Cuba na
kujaza mafuta, Castro aliwakubalia kwa sharti la mihadarati hiyo
isiuzwe ndani ya Amerika ya Kusini bali isafirishwe na kuuzwa Marekani
ambapo alisisitiza kuwa atafurahi akiona vijana wa mabepari wakiharibika
akili kwa mihadarati.
Baada ya Cocaine ya Pablo kuingia kwenye soko Marekani uhitaji na
biashara ya mihadarati ya Cocaine ilipaa kwa kasi ya ajabu na Pablo
Escobar akaanzisha rasmi genge lake la biashara ya mihadarati na
akaliita Medellíne Cartel. Ili kufanikisha usafirishaji wa mihadarati
yake kwa ufasaha na uhakika, Pablo alinunua ndege za mizigo 15 za ukubwa
wa kati na helikopta sita.
Pia alinunua nyambizi (submarines) ndogo. Hadi kufikia mwaka 1985 Pablo
alikuwa anasafirisha takriban tani 70 mpaka 80 za Cocaine kwa mwezi na
alikuwa ameshikilia asilimia 80 ya soko la mihadarati la Marekani.
Katika miaka ya 1990 utajiri wake ulifikia Dola za Kimarekani bilioni 30
na Jarida maarufu la Forbes lilimuorodhesha Pablo Escobar kama mtu
namba tano tajiri zaidi duniani.
Moja ya vitu muhimu vya kihalifu alivyovifanya Pablo na kufanikiwa
kuibuka kinara wa uhalifu Amerika ya Kusini ilikuwa ni kutekeleza sera
yake aliyoianzisha ili kuidhibiti serikali na vyombo vya ulinzi ambapo
sera hii aliita “Plata o Plomo” (fedha au risasi)). Akiwa na maana
kwamba kama wewe ni mtu wa serikali na ikitokea mmesigana basi atakupa
fedha (rushwa) kama ukikataa kupokea basi anakupiga risasi kwa kutumia
watu wake.
Aliwahi kukamatwa na alitoroka jela akawa anatafutwa. Baada ya mwaka
mzima wa msako mkali hatimaye Desemba 2, 1993 jeshi la Colombia
lilifanikiwa kunasa mawasiliano ya simu kati ya Pablo na wasaidizi wake.
Wakatumia ‘triangulation technology’ kung’amua mahali alipo katika Mtaa
wa Los Olivos katika mji wa Madellín. Baada ya kufanikiwa kufahamu
nyumba aliyojihifadhi pasipo kupoteza muda wakafanya shambulio la
kushitukiza. Mlinzi wa Pablo alipigwa risasi na kufariki papo hapo na
Pablo alipigwa risasi mguuni na akajikongoja mpaka juu ya paa.
Wanajeshi waliingia ndani walipanda juu ya paa na walimkuta Pablo
amelala chini amefariki dunia akiwa na tundu la risasi aliyopigwa kwenye
sikio na kutokea upande wa pili wa kichwa.
Marafiki zake wa karibu pamoja na kaka yake wa kuzaliwa wanasema kwamba
siku zote Pablo alikuwa anasema kuwa hatakubali kupigwa risasi ya mwisho
na adui yake, kama ikitokea ameshambuliwa na adui na hana namna ya
kujiokoa basi atajipiga risasi sikioni itokee upande wa pili.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa Pablo katika dunia hii kwa kifupi sana,
ndiye aliyesababisha leo Makonda afanye anayoyafanya katika Dar yake
mpya dhidi ya madawa ya kulevya.]
Post a Comment