0


Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Charles Mlingwa wamelipuliwa bungeni wakidaiwa  kutumia madaraka yao vibaya.

Tuhuma hizo zilitolewa jana na wabunge wa upinzani Conchesta Rwamlaza (Viti Maalum - Chadema) na Dk Godwin Mollel (Siha - Chadema) walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Rwamlaza alidai kuwa katika Kijiji cha Kamwila wilayani Muleba, Profesa Tibaijuka akiwa serikalini, aliomba eka 1,098 lakini hivi sasa anamiliki eka 4,000 jambo ambalo linazua mgogoro na wananchi.

“Hili linaleta matatizo kwa kuwa haiwezekani mtu awe na eneo hilo lote halafu anakodisha kwa wananchi,” alisema Rwamlaza.

Alisema kuna haja ya kwenda kupima ardhi hiyo na kama Profesa Tibaijuka aliomba heka 1,098 apewe hizo na si kumiliki eka 4,000 alizonazo hivi sasa.

Dk Mollel alimtaka Waziri Mkuu amhamishe Dk Mlingwa akidai ni tatizo katika wilaya hiyo.

Alisema juzi ulitokea mgogoro kati ya wananchi wa Arumeru na Siha katika mpaka jambo lilisababisha kubomoleana nyumba.

“Mkuu wa Wilaya alifika pale akiwa amelewa na kusababisha wananchi kuchukua hatua hizo wakati ilitakiwa tu tutumie akili,” alisema Dk Mollel.

Dk Mollel alisema kama DC huyo ataendelea kuwa na tabia hiyo, migogoro haitaisha na wawekezaji hawatawaheshimu wananchi kwa kuwa kiongozi wao anawaaibisha.

“Kama hamtamtoa huyu DC ambaye anatuaibisha kwa kuomba vitu vidogovidogo kwa wawekezaji basi sisi tutamtoa kwa kuwa hatuhitaji aibu.”

Alisema kuna haja ya kwenda kupima ardhi hiyo na kama Profesa Tibaijuka aliomba eka 1,098 apewe hizo na si kumiliki eka 4,000 alizo nazo hivi sasa.

Dk Mlingwa ajibu tuhuma
Akizungumzia tuhuma hizo, Dk Mlingwa alisema tangu kipindi cha kampeni, mbunge huyo alikuwa akimshambulia kwa maneno ya uongo ili kupata kura za huruma.

“Hata hii leo (jana) asubuhi alinitumia meseji akisema ooh nakwenda kukushtaki kwa Rais na Waziri Mkuu, akaweka na maneno ya vitisho mimi nikamwambia nenda kwa vile yote ni uongo,” alisema.

“Nadhani kwa sababu ya ahadi za uongo alizokuwa nazo kuwa akichaguliwa yeye mashamba yote ya wawekezaji yaliyoko Siha, yatakuwa mikononi mwa wananchi jambo ambalo haliwezekani.”

Dk Mlingwa alisema wawekezaji hao wana hati za kumiliki mashamba hayo na hilo ndilo ambalo Serikali imekuwa ikiwaeleza wananchi ukweli ili kuepuka propaganda za uongo za mbunge.

“Hiyo ndiyo imemfanya aendelee kumsema vibaya mkuu wa wilaya na mkurugenzi katika kila nafasi anayoipata hata hayo aliyoyasema bungeni ameniambia kwa meseji leo atayasema,” alisema.

“Mkuu wa wilaya kwa bahati nzuri hawezi kujificha tabia na matendo yake kama ningekuwa mlevi wananchi wangeshasema.”

Wabunge wamemshushia ‘zigo’ la migogoro ya ardhi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakimtaka atatue migogoro hiyo kwa kasi ambayo ameanza nayo.

Akichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, jana, Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alizungumzia mgogoro wa ardhi katika Wilaya ya Arumeru na kusema mgogoro huo umekuwapo tangu mwaka 1993.

Nassari alinukuu tangazo katika gazeti la Serikali na kusema Rais alitangaza kufuta umiliki wa shamba hilo. Hata hivyo, alisema mwekezaji huyo aliendelea kumiliki shamba hilo na kuwakataza wananchi kulima.

“Huyu Mzungu ni nani? Kwa nini anakuwa na nguvu kuliko Serikali? Rais alitangaza kufuta umiliki wa shamba hilo tangu mwaka 1993, lakini mpaka leo anaendelea kumiliki eneo hilo wakati halitumii,” alisema.

Alisema wananchi wanapodai ardhi yao wanafunguliwa kesi za kusingiziwa na kufungwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Bupe Mwakanata alimtaka waziri Lukuvi kushughulikia mgogoro wa shamba la Efatha, uliodumu kwa muda mrefu bila kutatuliwa.

“Serikali iwasaidie wananchi wake kwa kuwarudishia ardhi yao ambayo haitumiki kikamilifu. Wananchi wa eneo hilo wanategemea kilimo, ukiwanyang’anya ardhi unawasababishia ugumu wa maisha,” alisema.

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alizungumzia mgogoro katika eneo linalozunguka Ziwa Chala. Alisema eneo hilo amepewa mwekezaji ambaye anawazuia wananchi kutumia maji na kusababisha mgogoro kati ya wananchi na mwekezaji na kati ya wananchi na Serikali.

“Ziwa Chala ndiyo pekee ambalo asilimia 85 ya maji yake ni safi na salama na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wako pale kufanya utafiti. Tunaomba umalize mgogoro huo, ili wananchi watumie ziwa hilo na ardhi kwa ajili ya kilimo,” alisema Selasini.

Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), Moshi Kakoso alisema Mkoa wa Katavi una migogoro mingi ambayo inasababishwa na mipaka kati ya vijiji hivyo na Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Alisema vijiji vya Kapanga, Lugonesi, Kabage na Nkungwi vinakabiliwa na mgogoro ya ardhi ambayo inawafanya wananchi wa maeneo hayo kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji.

“Ninaomba wakati waziri anashughulikia migogoro ya ardhi atuangalie na sisi mikoa ya pembezoni. Tuna migogoro mingi ambayo haijapatiwa ufumbuzi na Serikali haijafanya jitihada zozote,” alisema.

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Omary Mgumba alisema kumekuwa na mgogoro kati ya Mkoa wa Morogoro na Pwani kwenye vijiji vya mpakani.

Alimtaka Waziri Lukuvi kutembelea eneo hilo ili mgogoro uishe na wananchi wafanye kazi ya uzalishaji.

Mbunge wa Karatu (Chadema), Willy Quambalo alisema kuna mwekezaji katika wilaya hiyo ambaye amepewa ekari 3,850 huku wananchi wakipata shida kwa sababu ameziba njia ambayo inapita katika eneo hilo.

Wakati huo huo, Lukuvi amepiga marufuku watu wote wenye mashamba makubwa ambao wanayapima na kuuza viwanja, waache kwa kuwa haliruhusiwi kuanzia sasa.

“Kama ni shamba litabaki kuwa shamba kama mtu alinunua shamba anataka kubadilisha liwe kiwanja imekula kwake,” alisema Lukuvi na kuongeza kama kuna mtu anataka kufanya hivyo akabidhi shamba kwa halmashauri ili ligawiwe au kuuzwa.

Post a Comment

 
Top