Vita dhidi ya ujangili inazidi kushika kasi baada ya kikosi kazi maalumu cha kupambana na ujangili kumnasa Mhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa tuhuma za ujangili.
Pia,
kikosi hicho kimemtia mbaroni Mchungaji wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG), wilayani Arumeru kwa tuhuma za kukutwa na jino
la tembo wakati akisaka mnunuzi.
Waziri
wa Utalii na Maliasili, Profesa Jumanne Maghembe alisema jana kuwa
vyombo vya ulinzi na usalama vimeongeza kasi ya kupambana na majangili
katika mapori yote ya akiba.
Meneja
Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete katika taarifa yake jana alisema
kuwa Mei 14, mwaka huu, shirika hilo lilipokea taarifa za siri kuwa
mchungaji huyo alikuwa akimiliki jino hilo.
“Tuliambiwa
mchungaji huyo alikuwa akihitaji mtu wa kufanya naye biashara. Baada ya
kupata taarifa tuliwasiliana na kikosi kazi maalumu cha kitaifa ili
wafuatilie,” alisema Shelutete.
Shelutete
alidai kuwa Mei 15, mchungaji huyo alikamatwa na kumtaja ofisa wa
Tanapa kuwa ni mmoja wa washirika wake katika biashara hiyo.
“Alipokamatwa na kuhojiwa alimtaja mhifadhi huyo kuwa anataarifa za yeye kuwa na jino hilo ndipo Mei 16 naye alikamatwa,” alisema Shelutete.
Tanapa
imewaomba raia wema kuendelea kufichua vitendo vya ujangili na
haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi wake watakaobainika
kujihusisha na ujangili.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita, Waziri Maghembe alisema majangili sasa wamehamishia
ujangili wao katika mapori ya akiba baada ya kudhibitiwa kwa kiasi
kikubwa katika Hifadhi.
Profesa
Maghembe alionya kuwa hakuna jangili hata mmoja ambaye atasalimika
katika msako unaoendelea na kwamba, salama yao ni kujisalimisha pamoja
na silaha zao.
Kukamatwa
kwa ofisa huyo mwandamizi wa Tanapa kumekuja miezi michache baada ya
kufikishwa mahakamani kwa Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia cha Mamlaka
ya Ngorongoro kwa tuhuma za ujangili.
Mtuhumiwa
huyo, Iddy Mashaka (49), anadaiwa kuwa Januari 6 na Februari Mosi
wilayani Meatu alimshauri mshtakiwa namba mbili, Shija Mjika (38) kuua
wanyama wasioruhusiwa.
Watuhumiwa
wengine ambao wanashitakiwa pamoja na Mkuu huyo wa Kitengo cha
Intelijensia, wao wameshitakiwa kwa kutungua helkopta na kumuua rubani
wake, Rogers Gower huko Maswi.
Post a Comment