0

Baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kueleza Bungeni kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alijimilikisha ardhi iliyotolewa kwa wananchi wilayani Monduli mkoani Arusha na kuahidi kuirejesha, Mwanasiasa huyo amejibu tuhuma hizo.

Lowassa amesema kuwa halijui shamba alilolizungumzia Waziri huyo na kwamba hakuna ardhi ambayo anaimiliki kinyume cha taratibu.

Alisema kuwa hana taarifa kamili kuhusu maelezo ya Waziri Lukuvi na kwamba ameomba Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga (Chadema) kulifuatilia kwa karibu na kumpa taarifa ili aweze kulitolea ufafanuzi.

“Nashindwa kutoa maelezo kuhusu taarifa hizo kwa sababu sifahamu lolote kuhusu shamba hilo,” Lowassa anakaririwa na gazeti la Jambo Leo lililofanya nae mahojiano kwa njia ya simu. 
“Mimi sipo Bungeni, nimesikia hizo habari, lakini sijui zimetolewa lini na nani. Mbunge wangu analifanyia kazi kwa sababu sina shamba nilalolimiliki ambalo liko kinyume na taratibu,” aliongeza.

Akijibu hoja ya Mbunge wa Monduli kuhusu umiliki na uporaji wa ardhi unaofanywa na vigogo jimboni humo, Waziri Lukuvi alieleza kuwa kuna shamba ambalo lilidhaminiwa na Rais Benjamin Mkapa ili wapewa wananchi jimboni humo, lakini  Lowassa alijimilikisha.

“Lile Shamba la Makuyuni lilitolewa kwa wananchi litarudi kwao na ukae ukijua litakuwa kwao kwa sababu aliyejimilikisha ni Edward Lowassa,” alisema Lukuvi na kuahidi kulirejesha mikononi mwa wananchi hao.

Post a Comment

 
Top