0


Jeshi la Polisi Nchini linawashikilia watuhumiwa 14 kufuatia tukio la mauaji ya watu watatu lililotokea katika msikiti wa Rahman eneo la Ibanda relini mkaoni Mwanza, Mei 18 mwaka huu.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo ili kufanikisha kuwakamata wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.

“Nitoe wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya usalama katika kufichua wahalifu kwa kuwa ni watu tunaoishi nao, hivyo hakuna budi kutoa taarifa zao ili usalama na mali zetu uendelee kuimarika”, aliongeza Kamishna Msaidizi Bulimba.

Hata hivyo, alieleza kuwa hali ya usalama nchini iko shwari na kuwatoa hofu wananchi kwamba jeshi hilo limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwepo.

“Niwaombe wananchi kuondoa hofu juu ya hali ya usalama na wasiwasi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu wanakamatwa haraka”, alisema Kamishna Msaidizi  Bulimba.

Aliongeza kuwa uchunguzi zaidi wa matukio ya uhalifu nchini unaendelea ikiwemo matukio ya mkoani Tanga, Dar es Salaam na mikoa mingine ili kubaini na kuwakamata wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hivi karibuni kumeripotia matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani katika mikoa mbalimbali  ikiwemo mauaji ya watu watatu waliouawa wakiwa msikitini jijini Mwanza.

Post a Comment

 
Top