Benki moja nchini
Kenya imewekwa chini ya mrasimu baada ya wateja kutoa pesa zao kwa wingi
kufuatia wasiwasi kuhusu uthabiti wa benki hiyo.
Benki Kuu ya Kenya (CBK), taasisi iliyo na jukumu la kusimamia huduma za benki Kenya, imeamua kuweka benki hiyo ya Chase Bank chini ya mrasimu ikisema benki hiyo ilishindwa "kutimiza masharti yake kifedha tarehe 6 Aprili”.
CBK imesema hatua hiyo imechukuliwa kwa maslahi ya „walioweka pesa kwenye benki hiyo, wanaoidai pesa benki hiyo na umma.”
Benki hiyo sasa itasimamiwa na shirika la Kenya Deposit Insurance Corporation (KDIC).
Gavana wa CBK Dkt Patrick Njoroge ameambia wanahabari kwamba Chase Bank haikuweza kutimiza mahitaji ya kimsingi kama vile „kuhamisha pesa za wateja”.
Matawi yote 62 ya benki hiyo nchini Kenya yalifungwa jioni, Dkt Njoroge akisema hatua hiyo ilitumiwa kuilinda benki hiyo baada ya wateja wengi kujitokeza kutoa pesa.
Jumatano, Chase Bank ilitangaza kwamba mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Zafrullah Khan na mkurugenzi mkuu Duncan Kabui walikuwa wamejizulu baada ya kuchapishwa kwa taarifa ya matokeo ya kifedha ya mwaka 2015.
Benki hiyo ilimteua Muthoni Kuria kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo na kuwahakikishia wateja wake kamba benki hiyo iliyohudumu kwa miaka 20 nchini Kenya ilikuwa imara.
"Tungependa kuuhakikishia umma kwamba pesa za wateja wetu na uwekezaji viko salama,” benki hiyo ilisema kupitia taarifa.
Gazeti la Business Daily la Kenya linasema taarifa mpya ya matokeo ya kifedha ya benki hiyo ilionesha kwamba jumla ya Sh8bn zilikopeshwa wakurugenzi wa benki hiyo bila kufichuliwa.
Taarifa hiyo mpya ilionesha wakurugenzi, washirika na wafanyakazi wa benki hiyo walikuwa wamekopa Sh13.62 bilioni badala ya Sh5.72 bilioni zilizokuwa zimetangazwa kwenye taarifa ya kwanza tarehe 31 Machi.
Benki hiyo ndiyo ya tatu kuwekwa chini ya mrasimu miezi ya hivi karibuni baada ya benki za Imperial na Dubai.
Benki ya National nayo iliwasimamisha kazi maafisa wake wakuu baada ya pesa zinazotengewa hatari kutokana na mikopo kupanda kutoka Sh525.3 milioni hadi Sh3.72 bilioni.
Hilo lilifanya matokeo ya kifedha ya benki hiyo kubadilika kutoka faida ya Sh2.2 bilioni baada ya kutozwa ushuru Septemba 2015 kuwa hasara ya Sh1.15 bilioni wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya kifedha ya mwaka wote.
Post a Comment