0

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
 
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesaini mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd, utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kufikishwa katika Kitengo Uratibu za Taarifa za Mikopo (Credit Reference Bureau) kilichopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
 Kampuni ya CreditInfo Ltd ina leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
 
Kufuatia makubaliano hayo yaliyotiwa saini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, mwanafunzi ambaye ataomba mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya kifedha hapa nchini, taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji huyo ni anastahili  na kama ana nidhamu ya kurejesha mikopo.
 
 Kwa mujibu wa mkataba huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kampuni ya CreditInfo ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji zinapatikana kwa taasisi zote za kifedha, ikiwamo mabenki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa mikopo mipya kwa wanufaika wa mikopo hiyo. 
 
“Heslb ina furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya kukopesheka na taasisi za kifedha,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Jerry Sabi, wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo jijini Dar es Salaam. 
 
Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd, Davith Kahwa, alisema lengo la kampuni hiyo ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinaongezeka na wakopaji wanakuwa na nidhamu kwa mikopo waliyopata. 
 
 “Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao wamekuwa wakilipa watapata fursa ya kipekee ya kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu wanayoionyesha kwa mikopo yao,” alisema Kahwa katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Meneja wa CreditInfo Tanzania, Van Reynders.
 
Hadi sasa, zaidi ya Sh. trilioni 2.1 zimetolewa na HESLB kwa wakopaji na kati ya fedha  hizo, Sh. bilioni 258 zimeiva na hivyo kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika. 
 
Kiasi kilichobaki kinajumuisha fedha walizopewa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo na ambao muda wa kuanza kuwadai (miezi 12 baada ya kumaliza masomo) haujafika.
CHANZO: THE GUARDIAN

Post a Comment

 
Top