Mbunge
wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), maarufu kwa jina la ‘Maji
Marefu’ amewalipua wabunge waliokosa ubunge katika kipindi hiki na
vilivyopita kwa kuhodhi nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini
Dodoma na kupangisha watu wengine kinyume cha utaratibu wa shirika
hilo.
Alisema
hali hiyo imefanya wabunge wapya, ambao ni asilimia 70 ya wabunge wote
kwa sasa, kukaa nyumba za kulala wageni wakati zipo nyumba hizo kwa
wabunge kulingana na mkataba na NHC.
Mbunge
alisema wapo watu wamepangishwa na wabunge hao wa zamani, ambao
wamegeuza nyumba hizo kama kitega uchumi kinyume na taratibu.
Ngonyani
alisema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akichangia mjadala wa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Alimuomba
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,
kufuatilia suala hilo na shirika kwa ujumla, aondoe wapangaji hao
waliowapangishia wengine kinyume cha utaratibu na kuwapatia nyumba
wabunge wapya ambao hawana nyumba za kuishi.
Alisema
wabunge hao waliokosa nafasi ya kurudi jimboni miaka tofauti, mkataba
wao wa kupangishwa nyumba hizo umekwisha, kwani ukishakosa ubunge hauna
dhamana tena mpaka utakaporudi.
“
Kuna wapangaji wengi ambao ni wabunge waliokosa nafasi hiyo ambao
wamepangishwa na shirika na badala yake hadi leo wamezishikilia nyumba
hizo hawataki kuziachia, ”alisema Ngonyani.
Alieleza
kuwa baada ya kukosa nafasi za ubunge na kushindwa kurudi bungeni,
wabunge hao walipaswa kurejesha nyumba hizo kwa shirika, ambalo ndilo
lenye mamlaka ya kupangisha na si wao kupangisha wapangaji wengine
kupitia mikataba yao.
Hata
hivyo, taarifa kutoka NHC, Dar es Salaam jana kuhusu nyumba hizo
zilifafanua kuwa hazikutengwa kwa ajili ya wabunge pekee, bali hata watu
wa kawaida na kila mtu anaingia mkataba binafsi na shirika.
Pia
zilieleza kuwa, nyumba hizo zilikodishwa awali kutokana na mahitaji ya
wabunge uliokuwapo na wapo walionunua, hivyo wana dhamana nazo.
Aidha
ilieleza kuwa ikiwa kuna mpangaji aliyepangisha mtu mwingine bila
kujali alikuwa mbunge au la, anakwenda kinyume cha utaratibu,
watafuatilia suala hilo.
Katika
hatua nyingine, Ngonyani alisema bungeni kuwa NHC imebadilisha dhana na
kutoka kwenye kujenga nyumba za bei nafuu, kusaidia wananchi wenye
uwezo mdogo sasa inafanya biashara, kwani inajiendesha kibiashara na si
kwa lengo la kuundwa kwake.
Mbunge
wa Kinondoni, Maulid Mtulya (CUF) alisema nyumba za shirika hilo
zimejengwa kwa ajili ya mabepari kwa sababu wananchi wa kawaida
kutozimudu kutokana na bei zake za kati ya Sh milioni 40 hadi milioni
60.
Mbunge
wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM) alitaka shirika lijenge nyumba
kulingana na uwezo wa watu wa eneo husika kutokana na kuwa wanajenga
nyumba za gharama kubwa.
Alisema
ujenzi huo uzingatie katika miji inayokua kuiweka katika mandhari nzuri
na wakazi wa maeneo husika kumudu kupanga na kununua.
Post a Comment