TCRA waagizwa matumizi kuidhinishwa na Hazina
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) imeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuangalia namna ya kupunguza matumizi yake na kuhakikisha matumizi yao yanaidhinishwa na Msajili wa Hazina.
Akizungumza jana Dar es Salaam baada ya kupitia ripoti ya hesabu za TCRA za mwaka 2013/14, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lolesia Bukwimba alisema TCRA imekuwa na matumizi
makubwa tofauti na maelekezo ya Msajili wa Hazina anayetaka matumizi ya shirika yasizidi asilimia 60 ya makusanyo.
Bukwimba alisema katika ripoti ya TCRA inaonesha kuwa mwaka 2013/14, TCRA walikusanya Sh 79,620,936,797 (bilioni 79.62) na matumizi yake yakiwa ni Sh 76,844,165,369 (bilioni 76.84) zikiwamo gharama za wafanyakazi Sh 18,602,566,205 (bilioni 18.60) na gharama za uendeshaji sh 19,993,673,663 (bilioni 19.99).
“Kamati yetu inakazi kubwa ya kuangalia matumizi ya taasisi na mashirika ya umma dhidi ya uwekezaji hivyo tunaangalia zaidi gharama za wafanyakazi na gharama za uendeshaji, kwa ripoti tuliyonayo TRCA inatakiwa kuangalia namna ya kupunguza matumizi yake na kile wanachotumia lazima kiidhinishwe na Msajili wa Hazina,” alisema Bukwimba ambaye ni Mbunge wa Busanda mkoani Geita.
Awali akijibu hoja hiyo ya kwa nini gharama za wafanyakazi zimekuwa kubwa na pamoja na mambo mengine zimelenga katika kutoa mafunzo, semina na safari, Mwenyekiti wa Bodi wa TCRA, Profesa Haji Semboja alisema hali hiyo inatokana na kuwa sekta hiyo ni ngeni, hivyo kuhitaji mafunzo zaidi kwa wafanyakazi.
“Tunasimamia sekta nyeti kwa uchumi na usalama wa nchi, sekta hii ni ngeni na teknolojia inakua siku hadi siku, hivyo ni lazima wafanyakazi wetu waende sambamba au zaidi ya teknolojia yenyewe. “Mfano makampuni ya simu kila wakati yanatoa teknolojia mpya ambayo kutokana na utandawazi zinafika hapa nchini kwa haraka, sasa ni lazima tuende sambamba na teknolojia hizo, kwani tukilala kidogo hali inaweza kuwa mbaya,” alisema Profesa Semboja.
Kuhusu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida aliyetaka kuacha kuwekeza kwenye majengo na badala yake ijikite katika shughuli zake za msingi, Profesa Semboja alisema ni lazima kuwa na majengo imara na wanayoyamiliki kutokana na kuwa na mitambo inayohitaji usalama na si ya kuweka katika majengo ya kupanga.
Aidha, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko alisema fedha zinazotolewa na TCRA kama gawio kwa serikali za Sh bilioni 1.7 kwa mwezi ni ndogo na kuwataka kuhakikisha wanapandisha kiwango hicho.
Post a Comment