Makamu wa Rais wa
Kenya William Ruto atafahamu leo iwapo kesi inayomkabili katika Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) itatupiliwa mbali.
Mwanahabari Joshua arap Sang, aliyeshtakiwa pamoja na Bw Ruto, pia atafahamu leo iwapo ana kesi ya kujibu.
Bw
Ruto anakabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuhamisha watu kwa lazima na
mateso yaliyotekelezwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2007.
Amekana mashtaka hayo na mawakili wake wanataka kesi hiyo itupiliwe mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Watu takriban 1,200 waliuawa wakati wa mapigano hayo.
Upande wa mashtaka umekabiliwa na changamoto kadha kwenye kesi hiyo dhidi yake.
Mwezi Februari, majaji katika mahakama hiyo waliizuia afisi ya mwendesha mashtaka kutumia ushahidi wa
mashahidi ambao tayari wamejiondoa.
Mashahidi kadha muhimu
walibadilisha taarifa zao za ushahidi, jambo ambalo waendesha mashtaka
wanasema lilitokana na vitisho na kuhongwa.
Mawakili wa Bw Ruto
wanasema anafaa kuondolewa kesi hiyo kwa sababu mashahidi wengi wa
upande wa mashtaka wamejiondoa au wakabadilisha taarifa zao asili za
ushahidi.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda amekiri kwamba
kujiondoa kwa mashahidi kumeathiri kesi dhidi ya naibu huyo wa rais
lakini anasisitiza kwamba bado kuna ushahidi wa kutosha wa kuendelea na
kesi hiyo.
Bw Ruto alikuwa kwenye mrengo tofauti na Bw Kenyatta wakati wa uchaguzi wa 2007
Msemaji mmoja wa ICC ameambia mwandishi wa BBC Anna Holligan mjini The Hague kwamba kuna mambo kadha ambayo yanaweza kutokea.
Majaji wanaweza kuondoa mashtaka yote dhidi ya Bw Ruto,
wanaweza kuutaka upande wa mashtaka ubadilishe mashtaka au wanaweza
kukataa tetesi za upande wa mshtakiwa na kuamua kesi iendelee.
Mwaka
2014, mwendesha mashtaka aliondoa mashtaka sawa dhidi ya Rais Uhuru
Kenyatta akisema mashahidi walikuwa wametishiwa na kubadilisha ushahidi
wao.
Hatima ya kesi hiyo sasa inaonekana kutegemea iwapo mwendesha
mashtaka alithibitisha kwamba ana ushahidi wa kutosha wa kupinga
msimamo wa upande wa mshtakiwa kwamba hana kesi ya kujibu.
Suala la kutumiwa kwa ushahidi wa mashahidi waliojiondoa huongozwa na Kanuni 68 ya Mkataba wa Roma, uliounda mahakama ya ICC.
Mawakili
wa William Ruto walisema haikuwa haki kwa sheria hiyo kutumiwa kwenye
kesi dhidi yake kwani mabadiliko ya kuruhusu kutumiwa kwa ushahidi wa
mashahidi waliojiondoa yalifanywa baada ya kesi dhidi yake na
mwanahabari Joshua arap Sang kuanza.
Jaji Judge Piotr Hofmanski
aliamua kwamba ushahidi wa mashahidi waliojiondoa ulitumiwa bila kuwapa
mawakili wa washtakiwa fursa ya kuwahoji mashahidi hao.
Alisema haingekuwa haki kwa ushahidi huo kutumiwa dhidi ya washtakiwa.
Bw Sang, anadaiwa kutumia vipindi vyake vya redio kupanga mashambulio baada ya uchaguzi.
Baada
ya majaji kuamua ushahidi wa mashahidi waliojiondoa haufai kutumiwa, Bw
Sang alisema hiyo ilikuwa „hatua moja kuelekea kwa uhuru wetu”.
Bw
Ruto na Bw Kenyatta walikuwa kwenye mirengo pinzani wakati wa uchaguzi
wa 2007 lakini waliunda muungano wa kisiasa na wakashinda
uchaguzi mkuu wa 2013.
Post a Comment