Kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari zaidi ya kilometa 10 kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine kutokana na mafuriko hayo yalisababishwa na mvua iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kusababisha barabara kujaa maji kiasi cha njia kushindwa kuonekana.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye alifika eneo la Chalinze Nyama kujionea hali halisi, aliwataka madereva kuchukua hadhari ya hali ya juu pindi wanapopita kwenye eneo lililojaa maji. Pia aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua bado zipo na zinaendelea kunyesha.
Mvua hiyo iliyonyesha usiku kucha, ilianza saa tatu usiku hadi asubuhi, imeharibu pia miundombinu ya barabara kwani nguzo za umeme katika maeneo kadha wa kadha pembezoni mwa barabara kuu katika Wilaya ya Chamwino eneo la Kijiji cha Chalinze Nyama zilionekana kuinama na kukaribia kuanguka.
Kulingana na maelezo ya wakazi wa kijiji hicho ambako magari yote yaliyoanza safari ya kutoka mjini Dodoma kwenda Dar es Salaam na Morogoro yalikwama baada ya maji mengi kusambaa juu ya daraja na kusababisha magari yashindwe kupita, walisema yalisababisha hofu kubwa kwa wenyeji na wasafiri pia.
Maji ya mafuriko hayo yaliyokuwa yakitiririka kutoka maeneo ya milimani Kata ya Hombolo yalianza kujaa barabarani na maeneo ya kuzunguka nyumba za wakazi wa Kijiji cha Chalinze Nyama, yakiwafanya wenyeji kukaa nje maeneo ya mwinuko wakiwamo akina mama na watoto wao wadogo pamoja na wazee.
Takribani kaya zisizopungua 100 na magari zaidi ya 1,500 yakiwamo mabasi ya abiria na malori yalizuiwa kuendelea na safari zao na askari wa usalama barabarani ili kuepusha kutokea kwa ajali au kusombwa na maji. Kwa kiasi barabara hiyo kuu ilifungwa kwa muda kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi saa tisa alasiri baada ya maji kupungua ndipo yaliporuhusiwa kuendelea na safari.
“Ilipofika saa nne hivi kuna basi lilijaribu kupita lakini likaserereka abiria wakatokea madirishani baada ya hapo hakuna gari ambalo liliruhusiwa kupita mpaka sasa,” alisema mkazi mmoja wa Chalinze Nyama.
Aidha, familia inayosadikiwa ni ya Shehe wa Msikiti wa Jumuiya ya Ahmaddiyya uliopo kijijini hapo jirani na barabara itokayo Dodoma kwenda Dar es Salaam, walijikuta nyumba yao imezungukwa na maji ya mafuriko hayo na kushindwa kutoka nje hadi Jeshi la Zimamoto kutoka Dodoma Mjini walipokuja kuwanusuru.
Familia hiyo ya mama na wanawe wanne wadogo, ilijikuta katika wakati mgumu, na mama huyo alisema hadi alfajiri hawakujua endapo maji yalizunguka nyumba yake na kusababisha hofu na wao kushindwa kutoka nje.
Pia mvua hiyo imesababisha miundombinu ya umeme hususani nguzo zinazosambaza umeme kwenye kijiji hicho kwenda hadi wilayani Kongwa kuanguka na kusababisha umeme kukatika tangu usiku huo wa saa tisa usiku hadi jana. Mafundi wa Tanesco walionekana wakifanya kila juhudi kurekebisha hali hiyo ili zisianguke katika maeneo ya watu.
Pia nyumba za wanakijiji wapatao 30 wa Kijiji cha Nzali, Kata ya Hombolo Wilaya ya Chamwino pia hawana mahali pa kuishi kutokana na athari za mvua hiyo. Hadi saa tisa alasiri, maji yalikuwa yakitiririka kwa wingi japo magari yalishaanza kuruhusiwa kuendelea na safari.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema serikali itahakikisha wananchi walioathirika wanapata huduma zote.
Post a Comment