Ni ule uliohusisha vigogo wa Serikali, Jeshi la Polisi
*Watumia bilioni 5/- mafunzo kwa watu watano
MKATABA tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Lugumi, umezidi kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kushindwa kuendelea na sakata hilo kutokana na kuhamishiwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hatua hiyo inatokana na utata uliogubika mkataba huo ambao unawahusisha vigogo kadhaa wa Jeshi la Polisi pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, huku ikidaiwa kuwa huenda ikawa njia ya ‘kulindwa’.
Wiki iliyopita PAC ilipokutana na jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14
zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibainika kuwa mwaka 2011 liliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Lakini hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 pekee na kampuni hiyo kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za makubaliano ya mkataba.
Kutokana na hali hiyo, PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya ufisadi katika tenda hiyo, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili wajumbe waweze kuupitia pamoja na kutoa maagizo.
Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA kuwa katika sehemu ya mkataba huo kati ya Jeshi la Polisi na Lugumi, imebainika kampuni hiyo kufanya mafunzo kwa watu watano ambayo wametumia Sh bilioni 5, huku mshauri mwekelezi akilipwa Sh bilioni 46 nje ya fedha zilizopo kwenye mkataba.
Hatua ya mkataba huo kupelekwa mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, inadaiwa kuwa njia ya kutaka kuwalinda baadhi ya vigogo ambao wanatajwa kuhusika na kashfa hiyo ambayo imelitia doa Jeshi la Polisi nchini.
“Hapa kuna kulindana tu, hakuna namna yoyote. Kama uchafu umebainika mbele ya Kamati ya PAC inakuwaje wengine wanadaka kitu ambacho hakikuanza kwao?
“Kuna kila dalili ya wingu na shaka, ila ukweli utajulikana tu, haiwezekani watu wanatumia fedha za walipakodi vibaya halafu inapokuja wanataka kushughulikiwa wanatafuta kivuli cha kujifichia,” kilisema chanzo chetu.
Mkataba huo uliibuliwa na PAC wiki iliyopita ambapo watendaji wa Jeshi la Polisi walishindwa kutoa maelezo ya kutosha ndipo ikawataka kuwasilisha taarifa juzi.
Pamoja na kutakiwa kufanya hivyo, hadi kufikia jana saa 10 jioni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, alisema kuwa kamati yao haijapokea taarifa yoyote kuhusu Kampuni ya Lugumi hivyo wameliandika barua Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo ndani ya siku tatu.
Alisema barua hiyo wamemuomba Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, ili aweze
kuwaandikia Polisi ili wawasilishe mkataba huo kwa mujibu wa utaratibu kama kamati ilivyoagiza.
“Hadi muda huu ninapozungumza nawe sijapata taarifa yoyote, kwa hali hiyo tumelazimika
kumwandikia barua Katibu wa Bunge ili awaandikie barua polisi walete mkabata huo ndani ya siku tatu kutoka leo (jana) kama walivyotakiwa na kamati yetu,” alisema Hilaly.
Post a Comment