WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameendelea kutesa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa anakopita kutafuta wadhamini akitafuta kuteuliwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa alianza kusaka wadhamini alipotua mkoani Mwanza wiki iliyopita ambako alipata mapokezi makubwa huku maelfu ya wana CCM wakijitokeza kumdhamini.
Hadi sasa Lowassa ametembelea mikoa ya Mwanza ambapo alidhaminiwa na wanachama 2676 , Geita, Mara, Mjini na Magharibi Zanzibar na Kaskazini na Kusini kisiwani Pemba.
Jana aliingia Mkoa Mara akitokea Mkoa wa Geita na kupata mapokezi makubwa katika uwanja wa ndege wa mjini Musoma saa 5.00 asubuhi.
Kabla hata Lowassa hajawasili Musoma, tayari watu wengi walikuwa wakimsubiri katika uwanja wa ndege, huku waendesha pikipiki (bodaboda) na magari mbalimbali yakiwa yamepangwa kwa ajili ya msafara wake.
Wanachama hao walimzuia Lowassa na msafara wake aliyekuwa akienda kwenye ofisi ya CCM mkoa huku wakitaka kwanza azungumze nao.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, aliwazuia akisema kanuni za chama kwa sasa haziruhusu Lowassa kuhutubia kwa vile muda wa kampeni bado.
Baada ya kutoka katika ofisi ya CCM mkoa, Lowassa alikwenda wilayani Butiama katika Kijiji cha Mwitongo nyumbani kwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Alipokewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Annarose Nyamubi na watoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka na Andrew na Chifu wa ukoo huo, Japhet Wanzagi.
Akiwa Mwitongo, mtoto wa Mwalimu Nyerere, Andrew, ndiye alizungumza kwa niaba ya familia kwa kumkaribisha Lowassa.
Hata hivyo Mama Maria Nyerere hakuwapo kwa kile kilichoelezwa na Madaraka Nyerere kuwa yuko Dar es Salaam kwa muda mrefu.
Lowassa na msafara wake walipata nafasi ya kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere kabla ya kutembelea msiba wa dada yake Mwalimu Nyerere, Tagaz na mpwa, John, waliofariki dunia juzi.
Msafara wazuiwa
Baada ya kutoka Butiama, msafara wa Lowassa ulielekea wilayani Bunda. Hata hivyo ilibidi usimame katika Kijiji cha Bitaraguru baada ya wana CCM na mashabiki kuusimamsha wakitaka azungumze nao.
Akizungumza na wana CCM hao, Lowassa aliwataka kumwombea katika safari yake ya matumaini.
“Asanteni kwa maokezi makubwa mliyonipa. Naomba mniombee mambo yangu yawe mazuri. Naenda na natamani kuwahutubia ila muda hautoshi, nitarudi mambo yatakapokuwa mazuri. Nawaomba wenye misalaba, rozari mpige magoti mniombee,” alisema Lowassa.
Lugola akoleza mapokezi
Akizungumza katika ofisi ya CCM Wilaya ya Bunda, Mbunge wa Mwibara, Alfaxard Kangi Lugola alisema, “wananchi wa wilaya hiyo wameacha kazi zao ili kuja kupakia gari lako la matumaini.
“Hii inanikumbusha maandiko ya Biblia ambako Yesu aliwauliza wanafunzi wake, Je, watu wananinenaje huko nje? Wanafunzi wake wakajibu, wengine wanakuita Eliya, wengine Yohana Mbatizaji. Akauliza tena, na ninyi mnaninenaje? Wakajibu, Wewe ni Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai.
“Tulipokuwa ofisini Lowassa uliniuliza lakini sasa umeona jinsi watu wanavyokunena hapa.”
Lugora alisema wananchi hao wameridhishwa na kazi ya Lowassa alipokuwa Waziri wa Maji ya kutoa maji kutoka ziwa Victoria kuyapeleka kwa wananchi.
Lowassa alipata wananchama 617 waliomdhamini.
Bunda ni jimbo la Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira ambaye pia amechukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM.
Hujuma Tarime
Wakati huohuo, baadhi ya wanachama wa CCM wilayani Tarime walizozana katika ofisi ya wilaya hiyo wakigombea kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kugombea urais kupitia chama hicho.
Lowassa aliingia wiilayani Tarime saa 9.00 alasiri na kuelekea katika ofisi hiyo ambako alipokelewa na umati mkubwa wana CCM na mashabiki.
Awali Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Barnabas Ilembe, alisema waliojitokeza kumdhamini Lowassa walikuwa 274 jambo lililofanya wanachama waliokuwa wamekusanyika ofisini hapo kulalamika wakikosoa takwimu hizo na wakidai hazikuwa za kweli.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya alisema ni hiari ya wanachama kumdhamini mtu wanayemtaka hivyo waachwe.
“Ni hiari ya wanachama kumdhamini mtu wanayemtaka. Kuna watu wanamhujumu Lowassa asidhaminiwe, hilo ni kosa kubwa katika chama. Wewe katibu huna mamlaka ya kuzuia watu,” alisema Sanya na kuongeza:
“Kama Katibu una mgombea wako sema kwa sababu ni kosa kwa kiongozi wa chama kuwa na mgombea mgongoni. Mimi nitaleta kila mtu kama nilivyomleta Lowassa”.
Baada ya kauli ya Sanya, katibu huyo wa wilaya alikabidhi fomu kwa Lowassa huku wanachama wakiendelea kulalamika wakitaka wapewe nafasi ya kumdhamini.
Post a Comment