0


MFANYABIASHARA anayetaka kununua hisa ndani ya Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameanza kasi ya kuitumikia klabu hiyo ya Simba kwa kuanza kulipa mishahara ya wachezaji kuanzia mwezi huu huku suala la kununua hisa likitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Hatua hiyo ya Mo imekuja baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kuridhia kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka wa sasa wa wanachama na kwenda kwenye mfumo wa hisa, kufuatia Mo kuhitaji kununua hisa asilimia 51.

Mohamed Dewji ‘Mo’ (kushoto)  akisalimiana na viongozi wa Simba.
Aidha, kamati itaandaa mkataba wa maridhiano ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake ambapo Mo alieleza kuwa ataisaidia timu hiyo huku akiwa anaendelea kusubiria mchakato wa hisa kukamilika.

Akizungumza na Championi Jumamosi, mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji Simba ambaye aliomba jina lake lifichwe, alisema Mo ataanza kuwalipa wachezaji mishahara kuanzia mwezi huu.
“Kwa sasa kuna kamati imepewa kazi ya kuwaelimisha wanachama juu ya suala hilo ili kuweza kufahamu faida gani watakayoipata juu ya suala hilo ili mwisho wa siku yafanyike maamuzi sahihi.


“Kwa kuanza, ataanza na kuwalipa mishahara wachezaji ambapo itaanzia mwezi huu na atapewa majina ya wachezaji wanaotakiwa kulipwa mishahara ili aweze kuwalipa wachezaji wote lakini jukumu alilopewa ni juu ya timu tu kwa sasa lakini mambo mengine yote yatabaki chini ya uongozi.
“Suala lake nadhani litachukua muda mrefu hata mwaka mmoja hadi kufikia kukamilika kwa mchakato mzima kufuatia kupata maoni mbalimbali na makubaliano kutoka kwa wanachama baada ya kupata elimu ya kutosha.

“Hata hivyo asilimia kubwa ya wanachama hawataki auziwe hisa kubwa ya asilimia 51 na badala yake auziwe asilimia 48,” alisema bosi huyo.

Alipotafutwa Msemaji wa Simba, Haji Manara kuzungumzia suala hilo, simu yake iliita bila ya kupokelewa hata katibu, Patrick Kahemele naye simu yake haikupokelewa.

Tayari Mo alishatoa msaada wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia usajili, kiasi ambacho Simba ilikitumia kwa ajili ya kukamilisha usajili wa wachezaji kadhaa nyota walionao hivi sasa.

Post a Comment

 
Top