0



VIGOGO wawili wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) wanaokabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2 wameachiwa kwa dhamana.

Washitakiwa hao ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani.

Hata hivyo, washitakiwa wengine akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu na wenzake watano wanaendelea kusota rumande.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Respicius Mwijage alitoa uamuzi huo jana kwa kuwa washitakiwa hao wawili hawaguswi katika mashitaka yaliyofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Alisema anakubaliana na hoja za upande wa utetezi zilizowasilishwa na Wakili Johnson Jamhuri kuwa mashitaka yanayowakabili washitakiwa hao yana dhamana na hayahitaji kuombewa dhamana hiyo Mahakama Kuu.

Hakimu Mwijage alisema, washitakiwa wanatakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya Sh mil 200, pia wawasilishe hati zao za kusafiria na hawatakiwi kwenda nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Post a Comment

 
Top