0


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amesema Tume ya Utumishi wa Mahakama imeamua kutangaza nafasi na ajira za majaji ili kuongeza uwazi katika ajira zao. 

Utaratibu huu mpya na wa kwanza kutumiwa na tume hiyo, nchini ulianza kutekelezwa jana baada ya gazeti la serikali la Habari Leo kuchapisha tangazo hilo, likianisha sifa za kitaaluma na uzoefu zinazohitajika na uzoefu wa waombaji na viambatanisho vya uthibitisho wa sifa hizo na uzoefu wa kitaaluma vinavyohitaji.

Akizungumza  kuhusu utaratibu huo, Jaji Chande ambaye ndiye mwenyekiti wa tume hiyo alisema wameamua kutumia utaratibu huo kuongeza uwazi, kupanua wigo na kuongeza ushindani ili kuwapata majaji wenye sifa.

Hata hivyo, Jaji Chande alisema utaratibu huo si kwamba ni mpya bali upo, kwa kuwa ni miongoni mwa taratibu za tume hiyo katika hatua ya kwanza ya upatikanaji wa majaji, yaani ya kupata orodha ya majina ya watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa majaji.

“Huu ni utaratibu wa tume, upo kwenye tume na tumekuwa tukiuongea mara kwa mara kwenye tume, lakini tulikuwa hatujautekeleza tu.

"Sasa safari hii tumeona ngoja tujaribu kupanua wigo kwa kutangaza,”alisema Jaji Chande.

Alifafanua kwamba katika taratibu za tume hiyo kupata majina ya kuingia kwenye mchakato wa kuteuliwa kuwa majaji kuna njia tatu ikiwamo ya tume yenyewe kuwasaka.

Njia nyingine ni kuziandikia taasisi za kisheria kama vile Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakuu wa vitivo vya sheria wa katika vyuo vikuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kutoa mapendekezo ya majina ya watu wenye sifa hizo.

Pia, alisema njia nyingine ni utaratibu wa kuwapandisha watumishi wa ndani ya mahakama, kama vile mahakimu wakazi na wasajili.

“Lakini pia, hili la kutangaza ni utaratibu wa nchi za Jumuiya ya Madola. Kuna kanuni kwamba uteuzi wa majaji uwe wa wazi ili kuongeza ushindani na ulenge uzoefu, umakini na ujuzi na uzingatie jinsia bila ubaguzi,” alisisitiza Jaji Chande.

Akizungumzia uzoefu wa nchi nyingine katika utaratibu huu wa kutangaza nafasi hizo, Jaji Chande alisema kuwa kuna nchi ambazo zimefanikiwa kuwapata majaji wenye sifa, lakini pia kuna nyingine hazikufanikiwa.

Alitoa mfano wa Kenya ambayo ilianza utaratibu huo kulingana na Katiba Mpya pamoja na Uingereza, lakini akasema Botswana licha ya kutumia utaratibu huo haikufanikiwa kuwapata watu wenye sifa kama ilivyokuwa ikitarajia.

Akizungumzia uteuzi wa majaji, Jaji Chande alisema kuwa hupitia katika hatua tano kabla ya hatua ya uteuzi wa mwisho ambao hufanywa na Rais.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kwanza hatua ya kupendekeza majina, ambayo hufanywa ama kwa watu kuomba au kupendekezwa na taasisi na mamlaka husika; hatua ya uchambuzi wa sifa na mafanikio yao na hatua ya usaili. 

Hatua ya nne, Jaji Chande alisema ni kupendekeza au kuandaa orodha ndogo na ya tano ni hatua ya uchunguzi ambayo hufanywa na vyombo mbalimbali vya dola, kama vile Usalama wa Taifa na vinginevyo.

“Baada ya hatua hizo, ndipo Rais hupelekewa orodha ya majina ya watu wenye sifa na kufanya uteuzi kutoka miongoni mwa majina hayo kulingana na idadi ya nafasi zilizopo. Kwa kila nafasi moja, yanatakiwa majina angalau matatu kwa nafasi moja,” alifafanua.

Kutokana na mchakato huo wa upatikanaji wa majaji, Jaji Chande alikanusha madai ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa wakati mwingine Rais huteua majaji wasio na sifa au ambao hawakupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Hakuna jaji aliyewahi kuteuliwa bila kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hiyo haijawahi kutokea. Majina yote yanapendekezwa na Tume na hakuna jina linaloteuliwa nje ya mapendekezo ya Tume kwani huo si utaratibu wa kikatiba,” alisema Jaji Chande.

Post a Comment

 
Top