0


Watuhumiwa wawili Zuberi Thabiti (30) na Iddy Adamu (32) wanaodaiwa kushirikiana kufanikisha tukio la kumbaka na kumdhalilisha binti wa miaka 21, mkulima (jina limehifadhiwa), mkazi wa Kata ya Dakawa, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, wamekamatwa na kohojiwa na jeshi la polisi mkoani humo.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo la kinyama usiku wa Mei 4, mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Titii iliyoko Dakawa ambapo Zuberi ambaye ni dereva, mkazi wa Mbarali Mbeya anadaiwa kumbaka binti huyo huku Iddy ambaye ni mkulima, mkazi wa Makambako akirekodi picha za video kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, baada ya kurekodi katika simu yake, baadaye Iddy alizituma picha hizo kwa mtu aliyefahamika kwa jina la Rajabu Salehe (26), mkazi wa Dakawa ambaye naye alizisambaza picha hizo katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa watu mbalimbali.

Taarifa ya polisi imeeleza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kwamba, binti huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Zuberi ambapo siku hiyo mtuhumiwa alimpigia simu binti huyo na kumwambia aende katika nyumba hiyo ya wageni.

Taarifa hiyo ya polisi imezidi kueleza kuwa, baada ya kufika katika chumba husika ndipo Iddy alipoingia kisha kumtaka binti huyo afanye atakachomuelekeza huku akimshikia kisu ili asipige kelele na baada ya kutekeleza ukatili huo (ubakaji), walimtaka asitoe siri hiyo vinginevyo atauawa.

Aidha, baada ya tukio hilo kuripotiwa kituo cha Polisi Dakawa Apliri 5, mwaka huu, polisi walianza uchunguzi mara moja ambapo walifanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 11 wakiwemo Zuberi na Iddy pamoja na walioshiriki kuzisambaza picha hizo za udhalilishaji ambao ni;

Rajabu Salehe (26), Saidi Athumani (26),  Musini Ngai (36), Saidi Mohamedi (24), John Peter (24), Hassani Ramadhani (27), Ramadhani Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjome (30), wote wakazi wa Dakawa ambapo kwa pamoja wamefunguliwa shitaka la PICHA ZA UTUPU (P.O.N.O.GRAFIA) chini ya kifungu cha 14 (1) (a) cha sheria ya makosa ya mtandao.

Taarifa hiyo ya polisi pia imeeleza kuwa jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine huku jeshi hilo likitoa onyo kwa wananchi wote kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kutoshiriki makosa ya uhalifu wa kimtandao kwani sheria itachukua mkondo wake.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu leo alikemea suala hilo bungeni na kueleza masikitiko yake makubwa kwa watu hao kutekeleza unyama huo na kusisitiza kuwa watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani haraka

Post a Comment

 
Top